• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Kinaya cha Sudi, Ng’eno katika jopo la nidhamu

Kinaya cha Sudi, Ng’eno katika jopo la nidhamu

Na DAVID MWERE

WABUNGE ambao wanafuatiliwa sana na Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kutokana na kutoa matamshi ya chuki sasa wametwikwa jukumu la kuhakikisha wenzao katika Bunge la Kitaifa wanadumisha nidhamu.

Wabunge Oscar Sudi (Kapsaret), Johana Ng’eno (Emurua Dikirr) na Didmus Barasa (Kimilili) ambao wamejipata pabaya kutokana na matamshi ya chuki, mnamo Alhamisi wiki jana waliteuliwa kama wanachama wa Kamati ya Nidhamu.

Kamati hiyo ambayo mwenyekiti wake ni Spika Justin Muturi na ina wanachama 14 na ina jukumu la kuhakikisha kuwa wabunge na wafanyakazi wa bunge wanadumisha nidhamu ya hali ya juu.

Uteuzi wa watatu hao hata hivyo, umeibua hisia kali kutoka kwa baadhi ya wabunge wakiuliza iwapo wana uwezo wa kuetekeleza majukumu yao katika kamati hiyo kutokana na rekodi yao mbovu ya nidhamu na misimamo yao ya kisiasa.

Naibu Spika Moses Cheboi ambaye pia ni mbunge wa Kuresoi Kaskazini na Kiongozi wa wachache John Mbadi walijitokeza na kusema wabunge hao hawafai kuhudumu katika kamati hiyo.

Akiwasilisha hoja ya kuunga uteuzi wa watatu hao, Bw Cheboi alisema ilikuwa kinaya kuwa watahudumu katika kamati hiyo ilhali wao ndio wanafaa warekebishwe nidhamu kuliko wengine.

“Huenda mienendo yao imekuwa mibaya wakiwa nje ya bunge lakini wanapokuwa hapa huwa wana nidhamu ya hali ya juu. Japo wao ndio wanafaa wahakikishe wana nidhamu kabla ya kuamua kesi ya wabunge wengine,” akasema Bw Cheboi na kuwachangamsha sana wabunge wenzake.

“Mmoja wao Johanna Ng’eno Kipyegon amekuwa mwenye nidhamu hapa ndani ya bunge. Hata hivyo, akiwa nje mambo huenda yakawa kinyume ila sisi tunazingatia sana mambo yanayotokea ndani ya bunge,” akaongeza Bw Cheboi.

Licha ya kuunga mkono hoja hiyo, Bw Mbadi alisema kuwa bunge ni asasi yenye heshima ya juu na hilo linafaa lizingatiwe wabunge wanapoteuliwa katika kamati ya nidhamu.

“Sudi, Ng’eno na Barasa wanafaa wafahamu kwamba wakiwa huko nje wanatazamwa kama wabunge ambao wanaafiki hadhi ya jumba hili. Kile ambacho unafanya kule nje kinatia doa hadhi ya bunge iwapo ni jambo baya,” akasema Mbunge huyo wa Suba Kusini.

“Hata katika hafla za mazishi watu watajiuliza inakuaje wabunge hawa ndio huwa kwenye kamati ya nidhamu ilhali wao ndio wanaongoza katika kurusha cheche kali za matusi dhidi ya wapinzani,” akasema Bw Mbadi.

Mabw Sudi na Ng’eno wanahudumu muhula wao wa pili bungeni na wamejipata pabaya mara kadhaa huku NCIC ikiwashutumu kwa kutoa matokeo ya uchochezi. Wawili hao wamewahi kukamatwa na kufikishwa kortini kwa madai ya kutoa matokeo ya uchochezi.

Bw Barasa anayehudumu muhula wake wa kwanza, naye alichunguzwa mnamo 2019 baada ya kudai kwamba baadhi ya wabunge walilipwa Sh5,000 ili kuangusha ripoti ya kamati ya bunge iliyogusia masuala ya sukari.

Hata hivyo, alikanusha madai hayo alipofika mbele ya kamati hiyo. Kando na hayo amejipata matatani na kitengo cha sheria kuhusu masuala ya maadili.

You can share this post!

Wakili wa Ruto achukua nafasi ya Bensouda

UDA yapigwa jeki uchaguzi Matungu