• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Kingi adai serikali ilinyakua ekari 237 za wenyeji

Kingi adai serikali ilinyakua ekari 237 za wenyeji

Na ALEX KALAMA

SERIKALI ya Kaunti ya Kilifi imesema uchunguzi wake umebainisha kuwa wasimamizi wa shamba la Shirika la Kustawisha Kilimo (ADC) walivuka mipaka wakaingilia shamba za wenyeji wa eneo la Magarini.

Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi alisema hayo yalibainishwa katika uchunguzi uliofanywa na masoroveya baada ya mzozo kutokea.

Akizungumza baada ya kukutana na Waziri wa Ardhi Farida Karoney mjini Malindi na kujadiliana kuhusu utata huo, Bw Kingi alisema wanatumai sasa ripoti hiyo itasaidia kukomesha mzozo ambao ulikuwepo.

“Ripoti iliyotolewa na masoroveya imebaini kuwa ADC imevuka mipaka na kuingia kwenye ardhi ya wakazi wa eneo hilo. Hatua hii huenda ikasaidia katika kutatua utata unaohusiana na shamba hilo,” alisema Bw Kingi.

Kulingana na gavana huyo, ADC imenyakua ekari 237 ya shamba za wenyeji baada ya kuvuka mipaka ya shamba la shirika hilo.Alisisitiza kuwa suala hilo linaathiri watu wengi kwa hivyo lazima kupatikane suluhu ya haraka ili kutuliza taharuki ambayo iliibuka.

“Afisi za ardhi kaunti hii zinatambua mipaka ya jadi kati ya wakazi na ADC na inaonekana wazi ADC imenyakua takriban ekari 237. Lazima tutalifuatilia swala hili ili suluhu ya haraka ipatikane,” alisema Bw Kingi.

Juhudi zetu kutafuta msimamo wa serikali kuu kuhusu suala hilo hazikufua dafu, kwani Bi Karoney hakuzungumza moja kwa moja na wanahabari baada ya mkutano wao.

Badala yake, aliamrisha maafisa husika kuwasilisha stakabadhi zote muhimu zinazohusu umiliki wa ardhi hiyo kwa afisi yake ili suala hilo lifuatiliwe kikamilifu. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro.

  • Tags

You can share this post!

Chanjo mpya ya Cuba kwa jina Abdala yaibua gumzo mtandaoni

Kivumbi chatarajiwa mahasimu Ujerumani, Uingereza wakivaana...