• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Kivumbi chatarajiwa mahasimu Ujerumani, Uingereza wakivaana raundi ya 16-bora

Kivumbi chatarajiwa mahasimu Ujerumani, Uingereza wakivaana raundi ya 16-bora

MAHASIMU Uingereza na Ujerumani watafufua uadui katika mojawapo ya mechi za raundi ya 16-bora za kudondosha mate baada ya mechi za makundi kukamilika Jumatano.

Ubelgiji anayochezea mvamizi matata Romelu Lukaku itapepetana na Ureno inayojivunia kuwa na supastaa Cristiano Ronaldo nayo Croatia anayotandazia kabumbu Luka Modric imekutanishwa na Uhispania iliyoaibisha Slovakia 5-0 na kuibandua kwenye Kundi E.

Vijana wa Gareth Southgate walifuzu bila kuhangaishwa kutoka Kundi D baada ya kulima Czech na Croatia 1-0 na kutoka sare tasa dhidi ya Scotland.Ujerumani iliteseka kabla ya kujikatia tiketi kutoka Kundi F.

Vijana wa kocha Joachim Loew walipoteza 1-0 dhidi ya mabingwa wa dunia Ufaransa na kulemea mabingwa watetezi Ureno 4-2 kabla ya kuponea tundu la sindano kuaga mashindano ikitoka 2-2 dhidi ya Hungary, Jumatano.

Hungary walikuwa wanabandua Ujerumani baada ya kuongoza 2-1 kupitia mabao ya Adam Szalai na Andras Schafer.Leon Goretzka aliokoa Ujerumani kwa kusawazisha 2-2 dakika ya 84 mjini Munich. Kai Havertz alifunga bao la kwanza la Ujerumani dakika ya 66.

Kitakuwa kivumbi Juni 29 kwa sababu Uingereza imepoteza mechi mbili pekee kati ya 26 zilizopita chini ya Southgate ugani Wembley nayo Ujerumani haijapigwa wala kufungwa bao mikononi mwa wapinzani hao katika mechi mbili zilizopita.

Mchuano kati ya Ureno na Ufaransa ulishuhudia penalti tatu zikifumwa wavuni katika sare ya 2-2 ugani Ferenc Puskas. Ronaldo aliweka Ureno kifua mbele kupitia penalti dakika ya 30 kabla ya Karim Benzema kupachika penalti ya kusawazisha sekunde chache zikisalia kipindi cha kwanza kitamatike.

Benzema alifungia Ufaransa goli la pili dakika mbili tu baada ya kipindi cha pili kuanza. Ureno ilinusurika kubanduliwa iliposawazisha kupitia kwa Ronaldo dakika ya 60. Ratiba ya 16-bora: Juni 26 – Wales vs Denmark (Amsterdam), Italia vs Austria (London); Juni 27 – Uholanzi vs Czech (Budapest), Ubelgiji vs Ureno (Seville); Juni 28 – Croatia vs Uhispania (Copenhagen), Ufaransa vs Uswizi (Bucharest); Juni 29 – Uingereza vs Ujerumani (London), Uswidi vs Ukraine (Glasgow).

  • Tags

You can share this post!

Kingi adai serikali ilinyakua ekari 237 za wenyeji

Shahbal akosoa dhana ya uvivu wa Wapwani