• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Kocha akana kuchafua watoto na ponografia

Kocha akana kuchafua watoto na ponografia

BRIAN OCHARO na MAUREEN ONGALA

KOCHA wa kandanda ameshtakiwa kwa kuwachafua watoto wawili na kuunda filamu ya ponografia ya vitendo hivyo.

Patrick Mbauni Muriithi almaarufu Pat Arve ama Coaches ama Daddy, anakabiliwa na mashtaka kadha ya unajisi, kushiriki kitendo kisichofaa na mtoto, ponografia ya watoto na ulanguzi wa watu.

Wahasiriwa wa unyama huo ni watoto walio na umri wa miaka 11.

Kwa mujibu wa mashtaka yaliyowasilishwa kortini, Bw Muriithi aliwanyanyasa kingono watoto hao katika nyumba yake ya kupanga Mwembe Tayari katika eneo la Kisumu Ndogo, Kaunti Ndogo ya Malindi.

Mshukiwa pia anadaiwa kushiriki kitendo kisichofaa na watoto hao kwa kuwagusa visivyo akitumia mikono.

Shtaka linaonyesha kuwa mtuhumiwa alitenda uhayawani huo tarehe mbalimbali kati ya Agosti 2022 na Januari 11, 2023.

Vilevile, Muriithi anakabiliwa na shtaka la ponografia ya watoto, ambapo serikali inadai alitengeneza video chafu za watoto hao kwa kutumia simu yake ya mkono.

Upande wa mashtaka ulisema mshukiwa alipatikana na video na picha chafu za watoto hao wawili kwenye simu yake hiyo ya rununu.

Inadaiwa aliunda video hizo za ngono Desemba 9 na 11 mwaka 2022.

Shtaka lingine analokabiliwa nalo ni la ulanguzi wa watu.

Serikali inadai mkufunzi huyo wa soka aliwapokea na kuwahifadhi watoto hao nyumbani kwake tarehe tofauti kati ya Desemba na Januari 11 mwaka huu, kwa madhumuni ya kuwanyanyasa kijinsia.

Mshukiwa, 28, alikana makosa hayo alipofikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Malindi, Bi Elizabeth Usui.

Afisa wa uchunguzi Sajini Wycliff Jefwa aliitaka korti imnyime mshtakiwa dhamana, akihoji kuwa ni mtu mwenye ushawishi katika jamii na huenda akawafikia mashahidi.

Kulingana na mpelelezi huyo, mshukiwa alianzisha klabu ya soka ya Pat Arve ambayo ameitumia kuwafanyisha watoto wadogo mazoezi.

“Mshukiwa ana uhusiano mkubwa na waathiriwa kiasi kwamba wanamtaja kama baba kwani hugharamia mahitaji yao. Hivyo, kuna uwezekano wa waathiriwa kushawishiwa vvisivyo,” Sajini Jefwa aliambia korti.

Aliongeza kuwa, mshtakiwa alishawishi wazazi wa watoto waruhusu akae nao, hivyo anaweza kuwachochea wasitoe ushahidi dhidi yake.

Korti iliamuru mshtakiwa arudishwe rumande kusubiri uamuzi wa dhamana. Kesi itatajwa Februari 7.

  • Tags

You can share this post!

TALANTA: Kwaya wembe kwa kueneza Injili na kukuza vipawa...

Korti yaamuru mwili wa Osugo ufanyiwe uchunguzi wa DNA...

T L