• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:43 AM
Korti yaamua Obure ana kesi ya kujibu sakata ya Sh1.3b

Korti yaamua Obure ana kesi ya kujibu sakata ya Sh1.3b

Na RICHARD MUNGUTI

WAZIRI Msaidizi wa Uchukuzi Chris Obure ana kesi ya kujibu kuhusiana na sakata ya Sh1.3 bilioni ya Anglo-Leasing iliyotokea akiwa waziri wa Fedha katika serikali ya Daniel arap Moi.

Mahakama Ijumaa ilisema kuwa Bw Obure pamoja na aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Uchukuzi Sammy Kyungu na Katibu wa Wizara ya Fedha Samwel Chamobo Bundotich, wana kesi ya kujibu kuhusiana na mashtaka ya uhalifu wa kiuchumi.

Aliyekuwa mkuu wa shirika la Posta, Bw Francis Mellops Chahonyo aliyeshtakiwa pamoja na Bw Obure, Bw Kyungu na Bw Bundotich aliaga kesi ikiendelea.

Akitoa uamuzi, Hakimu Mwandamizi, Bi Anne Mwangi alisema upande wa mashtaka umethibitisha washtakiwa hao wana kesi ya kujibu.

Bi Mwangi alisema kesi hiyo ilianza kusikizwa Oktoba 2015.

Upande wa mashtaka uliwaita mashahidi 27 waliowajumuisha maafisa wa serikali, wahasibu kutoka wizara ya hazina kuu na maafisa kutoka wizara ya uchukuzi.

Hakimu alisema kesi hiyo inatokana na mojawapo ya kandarasi 18 ambazo serikali iliipa kampuni ya Anglo-Leasing kununua vifaa vya hali ya juu ambazo zingelitumiwa na shirika la mawasiliano nchini.

Hata hivyo, ununuzi wa vifaa hivyo ulitibuka na kufanya serikali kupoteza mabilioni ya pesa.

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma alieleza mahakama mnamo Julai 11 2002 kuwa serikali ya Kenya ilitia sahihi mkataba na kampuni moja ya Amerika inayofahamika kama Spacenet Corporation kuuzia nchi hii vifaa vya mawasiliano vya thamani Dola za Kimarekani 11,787,000 (Sh1,301,284,800).

Vifaa hivyo vilikuwa vitumike katika shirika la Posta.

Mitambo iliyotazamiwa kununuliwa ilitambuliwa kwa jina la kiutaalam VSAT, mitambo ya kompyuta na vifaa vinginevyo.

Shahidi kutoka afisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu, Bw Evan Mwai alisema zabuni hiyo ya ununuzi wa vifaa hivyo haikukaguliwa na kuidhinishwa kulingana na mwongozo unaotambulika kisheria.

You can share this post!

Walimu Nairobi kula marupurupu ya juu ya nyumba

Sherehe za Mashujaa marufuku kaunti 46