• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
Walimu Nairobi kula marupurupu ya juu ya nyumba

Walimu Nairobi kula marupurupu ya juu ya nyumba

Na FAITH NYAMAI

WALIMU wanaofundisha katika shule zinazopatikana jijini Nairobi sasa wana kila sababu ya kutabasamu, baada ya Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC), kuwapatia marupurupu ya juu ya nyumba ikilinganishwa na wenzao katika kaunti nyingine.

Walimu wengine wanaofundisha katika miji mikubwa kama Mombasa, Kisumu, Nakuru, Thika, Nyeri, Eldoret, Kitale na Kisii pia watapata marupurupu ya juu kidogo ya nyumba.

Kwenye notisi iliyotolewa na TSC Ijumaa, walimu wakuu wa ngazi ya D5 sasa watalipwa marupurupu ya Sh50,000 jijini Nairobi kila mwezi huku wenzao katika manispaa wakilipwa Sh35,000.

Walimu wakuu wa shule nyingine katika miji midogo watapokea Sh25,000 huku waliosalia wakilipwa Sh20,000 kila mwezi.Mwalimu wa shule ya msingi ambaye anawekwa kwenye ngazi ya chini zaidi ya C1 atalipwa marupurupu ya nyumba ya Sh6,750 jijini Nairobi.

Wale wanaofundisha miji ya manispaa watalipwa Sh4,500, manispaa wengine 3,850 huku waliosalia wakilipwa Sh3,200.Aidha, walimu wanaowashikilia vyeo vya uongozi kama manaibu walimu wakuu, mwalimu mwandamizi na wale wanaoongoza idara mbalimbali nao watalipwa Sh45,000 kila mwezi.

Wale wanaofanya kazi kwenye manispaa watalipwa 28,000, wa miji mingine Sh21,000 na waliosalia Sh16,800.

Walimu wengine wa vitengo vingine nao watalipwa kati ya Sh35,000 na Sh4,200.

Waraka huo ambao ulitumwa mnamo Septemba 10, umenakiliwa kwa walimu wote, walimu wakuu wa shule za msingi, wale wa upili na wale wa taasisi za mafunzo.

Pia taasisi zinazotoa mafunzo kwa wasioweze kuona, wakurugenzi wa taasisi zinazotoa elimu spesheli na pia walimu wanaofundisha Hesabu, Sayansi na Masomo ya Kiteknolojia.Kulingana na TSC, mishahara haijabadilishwa pakubwa na mwalimu anayelipwa mshahara wa chini zaidi katika ngazi ya T- 5 ataendelea kupokea kati ya Sh21,756 hadi Sh27,195.

Mwalimu Mkuu anayelipwa ujira zaidi ngazi ya T- 15, Gredi 5 ambayo ni ya walimu wakuu wa shule za upili, atalipwa mshahara wa chini wa Sh131,380 na yule ambaye ataendelea kulipwa Sh131,380 huku anayelipwa pesa za juu zaidi akipokea Sh157,656 kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Bi Nancy Macharia alisema malipo hayo ni kulingana na makubaliano ya nyongeza ya mishahara (CBA) kati ya tume hiyo pamoja na Chama cha Walimu (Knut), Kuppet na Kusnet mnamo Julai 13.

Aidha walimu wanaohudumu katika mazingira magumu kikazi hasa maeneo kame nao watalipwa Sh6,000 kama marupurupu kwa wale kwenye kundi la B5 huku wa kundi D5 ambao hasa huwa ni walimu wakuu, wakipokea Sh38,100 kila mwezi.

Wiki jana, TSC iliwapandisha ngazi walimu 1,376 katika maeneo hayo kame huku wakiongeza walimu wengine ili kuwahudumia wanafunzi wa maeneo hayo.

TSC pia imesisitiza kuwa sera ya kuwahamisha walimu itazingatia hasa umbali wa wanandoa na ikahimiza walimu waendee chanjo ya virusi vya corona inayoendelea kutolewa hapa nchini.

You can share this post!

TAHARIRI: Usimamizi wa soka umedorora

Korti yaamua Obure ana kesi ya kujibu sakata ya Sh1.3b