• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Korti yazuia ‘kamata kamata’ za polisi

Korti yazuia ‘kamata kamata’ za polisi

Na BRIAN OCHARO

MAHAKAMA imeamua kuwa hatua ya maafisa wa polisi kukamata washukiwa na kuwasukuma kizuizini kabla wakamilishe uchunguzi wao ni haramu.

Jaji Reuben Nyakundi wa Mahakama Kuu ya Malindi alisema, mtindo huo ni ukiukaji wa haki za binadamu zilizolindwa kikatiba.

Katika uamuzi wake, alisema polisi wanafaa kukamilisha kusaka ushahidi wanaonuia kutumia katika kesi kabla wakamate washukiwa.

“Mtindo wa kukamata washukiwa kabla upelelezi uanze ni kinyume cha sheria na ukiukaji wa haki za kimsingi za binadamu na uhuru wao waliopewa kikatiba,” akasema jaji huyo.

Alikuwa anatoa uamuzi katika kesi ambapo watu watano walielekea mahakamani kuomba agizo litolewe ili wasikamatwe na polisi kuhusu mzozo wa ardhi.

Jaji Nyakundi alisema mahakama zimekuwa zikipokea maombi mengi kutoka kwa polisi ambao hutaka washukiwa waendelee kuzuiliwa uchunguzi unapoendelea, akisema hilo huwa halistahili kisheria.

Kulingana naye, polisi wamekuwa na tabia ya kutaka kuwanyima washukiwa na washtakiwa uhuru wao kabla upelelezi kuhusu kesi za uhalifu haujakamilika. Alisema hilo ni mojawapo ya changamoto ambazo zimekuwa zikiathiri huduma za mahakamani kitaifa.

“Ni muhimu kwa mahakama kufanya utathmini wa masuala yote yanayohusu kukamatwa kwa mshukiwa, hasa polisi wanapowakamata bila kuwepo kwa agizo la mahakama. Inafaa kuwe na sababu za kutosha na kuridhisha kuelezea sababu mtu anashukiwa kuhusika katika uhalifu. Haitoshi kusema kuwa mshukiwa ana mienendo fulani inayotiliwa shaka,” akasema.

Kwa msingi huu, mahakama inahitaji polisi kukusanya ushahidi kuhusu uhalifu kisha wakamate washukiwa, wala sio kukamata ndipo waanze kutafuta ushahidi dhidi yao.

Uamuzi wa Jaji Nyakundi huenda ukatumiwa na wananchi wengine ambao hulalamikia kukamatwa kwao na kuekwa kizuizini bila sababu, ambapo polisi huelekea mahakamani baadaye kuomba muda zaidi wa kukamilisha uchunguzi.

Katika kesi ya jana, Mabw Omar Kahindi, Elisha Kahindi, Martin Gona, Katana Patrick na Samuel Ngolo walipewa dhamana ya Sh100,000 ili kuzuia polisi kuwakamata.

You can share this post!

Rigathi hatimaye nje kwa dhamana ya Sh12 milioni

Sitishiki hata ukinitimua Wiper, Kibwana aambia Kalonzo