• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 8:50 AM
Sitishiki hata ukinitimua Wiper, Kibwana aambia Kalonzo

Sitishiki hata ukinitimua Wiper, Kibwana aambia Kalonzo

Na PIUS MAUNDU

KATIKA kile kilichoonekana kama hatua ya kumdhihaki kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana sasa amemtaka kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka amtimue chamani baada ya kukataa kufika mbele ya kamati ya nidhamu kujibu madai ya kuwa mkaidi.

Chama cha Wiper kimemtaka afike mbele ya kamati ya nidhamu kuelezea ni kwa nini hajakuwa akitoa mchango wake wa kila mwezi kwa chama na sababu yake ya kupigia debe mpinzani katika uchaguzi mdogo wa Wadi ya Kitise/Kithuki, Kaunti ya Makueni, mwezi uliopita.

Prof Kibwana ambaye amegeuka hasimu wa kisiasa wa Bw Musyoka, alipuuzilia mbali madai hayo.

Alisema mkataba baina chama chake cha Muungano na Wiper, umeelezea wazi kuhusu namna vyama hivyo viwili vilifaa kushirikiana.

Bw Musyoka tayari ametangaza kuwa amevunja mkataba kati ya chama cha Wiper na Muungano wa chama chake Gavana Kibwana.

“Wiper wanifanyie chochote wanachotaka lakini sitafika mbele ya kamati ya nidhamu,” akasema Gavana Kibwana huku akisema anaendelea kupona baada ya kufanyiwa upasuaji miezi miwili iliyopita.

Kiongozi huyo wa Makueni alisema hayo alipotembelewa na wazee waliofika nyumbani kwake kumjulia hali.

Wazee hao kutoka vuguvugu la Thome wa Akamba walielezea masikitiko yao kuhusu vita vya ubabe wa kisiasa vilivyopo miongoni mwa viongozi wa Ukambani.

Wazee hao walimtaka Bw Musyoka, Prof Kibwana na Gavana wa Machakos Alfred Mutua ambaye ametangaza kuwa atawania urais 2022, kuendesha kampeni zao kwa amani bila kuzozana.

You can share this post!

Korti yazuia ‘kamata kamata’ za polisi

Poghisio ataka Lonyangapuo kuhama Kanu