• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Krusedi ya Pasta Ezekiel yafutiliwa mbali Tanzania

Krusedi ya Pasta Ezekiel yafutiliwa mbali Tanzania

Na ALEX KALAMA 

Mchungaji Ezekiel Odero wa kanisa la New Life Kaunti ya Kilifi amepata pigo baada ya mkutano wake wa injili ambao ulikuwa umepangwa kufanyika jijini Arusha, nchini Tanzania kufutiliwa mbali na serikali ya nchi hiyo.

Kulingana na gazeti la Mwananchi nchini humo, serikali ya wilaya ya jiji la Arusha mnamo Jumapili Julai 16 ilifutilia mbali kibali cha mkutano wa injili kwa kile walichotaja kuwa Pasta Odero kuhusishwa kwenye tuhuma za vifo vya waumini wa kanisa lake humu nchini.

Mkutano huo ulikuwa ufanyike kwa siku tatu mfululizo katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Ngarenaro.

Ulikuwa umepewa jina “Siku Tatu za Kubadilishwa na Mungu” ambao ulikuwa unafaa kuanza Jumapili ya Julai 16 hadi Julai 18 2023 ulisitishwa ghafla saa chache tu baada ya mamia ya watu ambao walikuwa wamejitokeza katika uwanja huo wa shule tayari kuanza maombi kuagizwa na maafisa wa polisi nchini humo kuondoka mara moja.

Aidha, magazeti nchini humo yameripoti kuwa mkurugenzi mkuu wa jiji hilo la Arusha Bw Juma Hamsini alichukua hatua hiyo baada ya kugundua kuwa utaratibu wa kutoa kibali cha kuruhusu kufanyika kwa mkutano huo zilikiukwa huku akidai kuwa ofisi yake haikujulishwa kuhusu mkutano huo.

“Utaratibu wa barua zote za jiji ni lazima zianze kwa mkurugenzi mkuu, lakini kilichotokea ni kuwa barua ilikuwa inashughulikiwa na ofisi ya utamaduni na hadi kutokea kibali kwa niaba yangu bila ya mimi kujua,” ilisema taarifa yake katika gazeti la Mwananchi.

 

Pasta Ezekiel pia anadaiwa kuwa na ushirikiano wa kibiashara na mhubiri tata Paul Mackenzie wa kanisa la Good News International ambaye anadaiwa kushawishi waumini wake kufunga kula na kunywa hadi kufa kwa kisingizio cha kukutana na Yesu.

Mackenzie kwa sasa bado yuko kizuizini kwa madai ya kuchangia vifo zaidi ya 400 vya waumini wake waliozikwa katika hali tatanishi kwenye msitu wa Shakahola, Kilifi.

Mnamo mwezi Mei 2023, mhubiri Ezekiel Odero pia alikamatwa na kufikishwa katika mahakama kuu ya Shanzu kwa madai ya kuhusika na vifo vya waumini wake ambavyo vinadaiwa vilikuwa vikitokea katika kanisa lake ambavyo inasemekana viliripotiwa katika mochari na taasisi mbalimbali.

Akiwa katika mahakama kuu ya Shanzu, hakimu Joe Omido alimuachilia kwa dhamana ya Sh3 milioni au Sh1.5 milioni pesa taslimu.

 

  • Tags

You can share this post!

Panya wamejaa katika hospitali za Kaunti ya Murang’a –...

Raila na Kalonzo wapokonywa walinzi

T L