• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Kuppet yataka walimu wapewa mafunzo ya CBC

Kuppet yataka walimu wapewa mafunzo ya CBC

Na GEORGE SAYAGIE

CHAMA cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET) kinaitaka Wizara ya Elimu iwape mafunzo walimu wa shule za upili ili nao wawafundishe wenzao wa shule za kiwango cha chini Mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC).

Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori alisema chama hicho hakijaridhishwa na jinsi ambavyo wizara imekuwa ikishughulikia suala la utekelezaji wa CBC.

Bw Misori anadai kuwa Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amejihusisha sana ujenzi wa madarasa na kuimarisha miundomsingi ya shule mbalimbali badala ya kuwapa walimu mafunzo.

Bw Misori alisema walimu wanafaa wafundishwe jinsi watakavyoitekeleza CBC kwa wanafunzi wa Gredi ya Saba na Nane mnamo Aprili ili watoe mafunzo ya kiuhakika kwa wanafunzi wao.

“Walimu wa shule za upili bado hawapo tayari kuwafundisha wanafunzi wa Gredi ya Saba na Nane kwa sababu serikali bado haijawafunza. Tunamwomba Profesa Magoha aipe kipaumbele mafunzo ya CBC badala ya kujenga tu madarasa na kuimarisha miundombinu,” akasema Bw Misori.

Alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Narok mnamo Jumanne akiwa ameandamana na maafisa wa Kuppet.

Afisa huyo aliongeza kuwa imesalia miezi michache kabla ya wanafunzi kuanza masomo kwenye sekondari ya chini ilhali Profesa Magoha hamakinikii kuwapa mafunzo walimu ambao wataushughulikia mtaala huo.

Kuelekea mwisho wa mwaka jana, serikali iligharimia mafunzo ya walimu wa CBC kote nchini kwa gharama ya Sh3.4 bilioni kama njia ya kujiandaa kwa kipindi hicho cha mpito.

Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Dkt Nancy Macharia alisema walimu 229,292 wa shule za msingi za umma na za kibinafsi wamepokea mafunzo ya CBC pamoja na wakufunzi 1,166 kutoka Chuo cha Walimu.

Kwa mujibu wa TSC, mafunzo kwa wanafunzi wa gredi ya sita yalifanyika mnamo Disemba mwaka jana na inalenga kuwafundisha walimu 60,000 wa shule za upili mnamo Machi na Aprili.

“Masomo ya Gredi ya Saba na Nane yataanza hivi karibuni ila hakuna mwalimu ambaye amefundishwa kuwashughulikia wanafunzi,” akasema Bw Misori.

Kauli yake inakuja wakati ambapo serikali imekuwa ikiwasukuma wanakandarasi wakamilishe ujenzi wa madarasa kabla ya kuanza kwa mitihani ya kitaifa mnamo Machi.

You can share this post!

AFCON: Salah kuvaana na Mane kwenye fainali baada ya Misri...

CA yataka watangazaji wagombeaji kuacha kazi kufikia Aprili...

T L