• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
AFCON: Salah kuvaana na Mane kwenye fainali baada ya Misri kudengua wenyeji Cameroon kwenye nusu-fainali kupitia penalti

AFCON: Salah kuvaana na Mane kwenye fainali baada ya Misri kudengua wenyeji Cameroon kwenye nusu-fainali kupitia penalti

Na MASHIRIKA

KIPA Mohamed Abou Gabaski ndiye aliibuka shujaa wa Misri baada ya kupangua penalti mbili na kusaidia kikosi chake kukomoa Cameroon 3-1 na kufuzu kwa fainali ya makala ya 33 ya Kombe la Afrika (AFCON) mwaka huu.

Mshindi wa mechi hiyo iliyosakatwa Alhamisi usiku aliamuliwa kupitia penalti baada ya pande zote mbili kuambulia sare tasa chini ya dakika 120.

Misri ambao ni mabingwa mara saba wa taji la AFCON, sasa watakutana na Senegal wanaowania taji hilo kwa mara ya kwanza katika historia. Senegal ambao wanaorodheshwa wa kwanza barani Afrika na wa 20 kimataifa kwa mujibu wa viwango bora wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), waliwahi pia kutinga fainali ya AFCON mnamo 2002 na 2019.

Mechi ya fainali kati yao na Misri itakuwa fursa kwa Sadio Mane wa Senegal na Mohamed Salah ambaye pia anachezea Liverpool ya Uingereza kuvaana dhidi ya mwingine. Fainali hiyo itachezewa ugani Olembe jijini Yaounde mnamo Februari 6, 2022; siku moja baada ya wenyeji Cameroon kumenyana na Burkina Faso katika gozi la kutafuta mshindi nambari tatu nan ne.

Cameroon ambao ni mabingwa mara tano wa AFCON, walianza mechi yao dhidi ya Misri kwa matao ya juu na wakashuhudia makombora mawili ya Michael Ngadeu-Ngadjui na Samuel Gouet yakigonga mwamba wa lango la Misri waliomtegemea sana Salah na Mahmoud Trezeguet katika safu ya mbele.

Gabaski alipangua penalti za Harold Moukoudi na James Lea Siliki huku Clinton N’Jie wa Cameroon naye akipiga nje mkwaju wake. Mechi hiyo ilikamilika bila Misri kujivunia huduma za kocha wao Carlos Queiroz aliyeonyeshwa kadi nyekundu kwa kumkaripia msaidizi wa refa baada ya Wael Gomaa kuadhibiwa kwa kucheza visivyo.

Gomaa sasa atakosa pia mchuano wa fainali kwa kuwa alionyeshwa kadi nyingine ya manjano dhidi ya Morocco kwa kucheza kivoloya.

Ushindi wa Misri uliwawezesha kulipiza kisasi dhidi ya Cameroon walioshuka dimbani wakijivunia rekodi ya kushinda The Pharaohs mara tano ikiwemo kwenye fainali ya AFCON 2017 ambapo walishinda 2-1 jijini Gabon.

Misri walifuzu kwa nusu-fainali baada ya kukomoa Morocco kwa mabao 2-1 jijini Yaounde. walihitaji penalti 5-4 ili kudengua wafalme mara mbili, Ivory Coast, kwenye hatua ya 16-bora. Masogora hao wa kocha Queiroz  walianza kampeni za Kundi D kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Nigeria kabla ya kutandika Guinea-Bissau na Sudan 1-0.

Cameroon wanaowinda taji la AFCON kwa mara ya sita, walifungua kampeni zao za Kundi A kwa kutandika Burkina Faso 2-1 kabla ya kupepeta Ethiopia 4-1 na kusajili sare ya 1-1 dhidi ya Cape Verde. Walibandua Comoros katika hatua ya 16-bora kwa mabao 2-1 kabla ya kucharaza Gambia 2-0 kwenye robo-fainali.

“Mashabiki walikuwa na matarajio makubwa kwa sababu fainali hizi zinachezewa nyumbani. Walikuwa na kila sababu ya kutarajia taji kwa sababu ya rekodi nzuri ya Cameroon kwenye fainali za mashindano haya. Lakini chochote kinaweza kufanyika katika soka,” akasema kocha wa Indomitable Lions, Antonio Conceicao.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Uzinduzi wa programu ya kutega uchumi

Kuppet yataka walimu wapewa mafunzo ya CBC

T L