• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Maafisa sita wa polisi wakataa mawakili sita walioteuliwa na jaji mkuu Martha Koome kuwatetea katika kesi ya mauaji ya ndugu wawili

Maafisa sita wa polisi wakataa mawakili sita walioteuliwa na jaji mkuu Martha Koome kuwatetea katika kesi ya mauaji ya ndugu wawili

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA sita wa polisi wanaoshtakiwa kwa mauaji ya ndugu wawili kaunti ya Embu Agosti 1, 2021 waliwakataa mawakili sita walioteuliwa na Jaji Mkuu Martha Koome kuwatetea.

Badala yake maafisa hao sita Koplo Corporal Benson Mbuthia Mabuuri, Koplo Consolata Njeri Kariuki,Martin Musamali Wanyama, Nicholas Sang Cheruiyot, Lilian Cherono Chemuna na James Mwaniki Njohu walimrudia wakili Danstan Omari.

Bw Omari anawatetea washtakiwa hao sita pamoja na mawakili wengine tisa.Kwa jumla mawakili 10 wanawatetea washtakiwa hao sita.Mnamo Septemba 2, 2021, Bw Omari na wenzake tisa walijiondoa kwenye kesi hiyo Jaji Daniel Ogembo alipotupilia mbali ombi la kusitisha kushtakiwa kwa polisi hao kwa mauaji.

Bw Omari alikuwa ameomba mahakama isubiri matokeo ya ombi alilowasilisha katika mahakama ya kuamua kesi za ukiukaji wa haki.Lakini Jaji Weldon Korir alitupilia mbali kesi hiyo akisema,“siwezi sitisha kusikizwa kwa kesi iliyoko mbele ya jaji tunayetoshana mamlaka na nguvu.”

Kufuatia agizo hilo Bw Omari alikoma kuendelea na kesi aliyokuwa ameiwasilisha akisema chini ya kifungu cha sheria nambari 387n uchunguzi kubaini kilichosababisha vifo vya wavulana hao waliokuwa wanasoma vyuo vikuu.Kesi hiyo ilipotajwa tena mbele ya Jaji Ogembo aliamuru washtakiwa wasomewe mashtaka ndipo Bw Omari na wenzake walijiondoa.

Maafisa sita wa polisi kuanzia kulia Koplo Corporal Benson Mbuthia Mabuuri , Koplo Consolata Njeri Kariuki,Martin Musamali Wanyama, Nicholas Sang Cheruiyot, Lilian Cherono Chemuna na James Mwaniki Njohu wanaoshtakiwa kwa mauaji ya Emmanuel Mutura na Benson Njiru….Picha/RICHARD MUNGUTI

Baada ya abautani hiyo ya mawakili wao kujiondoa washtakiwa waliomba wapewe muda watafute mawakili wengine wawatetee katika kesi hiyo.Lakini Jaji Ogembo aliamuru naibu wa msajili katika kitengo cha kusikiza kesi  za uhalifu kiwateue mawakili watakaolipwa na mahakama kuwatetea washtakiwa hao sita.

Mawakili sita waliteuliwa na kuwatembelea washtakiwa katika kituo cha Polisi cha Capital Hill kuwahoji.Mbele ya Jaji Ogembo mawakili hao sita walisema ,“tuliwahoji washtakiwa na tukawaandaa kujibu mashtaka dhidi yao.”Lakini Bw Omari na wenzake tisa waliagizwa tena na washtakiwa hao sita waendelee kuwatetea.

“Kwa vile mmekataliwa na washtakiwa hii mahakama haiwezi kuendelea kuwashikilia kwa hii kesi. Jiondoeni,” Jaji Ogembo aliwaambia mawakili hao sita.Kabla ya kung’atuka mawakili hao sita walioteuliwa na Jaji Mkuu kuwatetea washtakiwa hao “ walinung’unika vikali wakisema muda wao uliharibiwa.”

Lakini Jaji Ogembo akawakumbusha Katiba inasema kila mshtakiwa atatetewa na wakili aliyejichagulia.Punde tu baada ya mawakili hao sita kuaga kesi hiyo , Bw Omari na wenzake waliwasilisha ombi lingine wakipinga washtakiwa wakishtakiwa kwa mauaji.

Jaji Ogembo alitupilia mbali ombi hilo na kuamuru washtakiwa wazuiliwe katika magereza ya Viwandani na Langata.Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 22, 2021 ombi lao la kuachiliwa kwa dhamana itakaposikizwa.Maafisa hao sita wa polisi waliokuwa wakihudumu katika kituo cha polisi cha Manyatta walitiwa nguvuni Agosti 14, 2021 kufuatia vifo vya Emmanuel na Benson.

Sita hao walikuwa wamewashika Emmanuel na Benson kwa makosa ya kukaidi sheria za kafyu.Wahasiriwa hao walikuwa wamekamatwa pamoja na watu wengine wanane waliofikishwa kortini  Agosti 2,2021.Polisi hao wamedai Emmanuel na Benson walijirusha kutoka kwa gari la polisi wakipelekwa kituo cha polisi cha Manyatta.

Washtakiwa wamesema wawili hao walianguka na kupata majeraha yaliyopelekea kuaga kwao.Wanaomba mahakama iamuru uchunguzi wa kubaini kilichosababisha vifo hivyo badala ya wao kufunguliwa mashtaka ya mauaji.Wanasisitiza Emmanuel na Benson walijinyonga kwa kujirusha gari la polisi likienda kasi.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya kusisimua Diamond League Omanyala akishirikishwa...

Wanaoshtakiwa kuua afisa wa KDF waachiliwa kwa dhamana