• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Wakenya kusisimua Diamond League Omanyala akishirikishwa mara ya kwanza

Wakenya kusisimua Diamond League Omanyala akishirikishwa mara ya kwanza

Na CHRIS ADUNGO

MKENYA Ferdinand Omanyala, 28, atanogesha leo kivumbi cha Diamond League kwa mara ya kwanza katika mbio za 100m kwenye duru ya Brussels ugani Van Damme Memorial Ubelgiji.

Nyota huyo aliyetinga nusu-fainali zilizopita za Olimpiki jijini Tokyo, Japan amekuwa katika fomu nzuri zaidi mwaka huu na amevunja rekodi ya kitaifa mara mbili.

Alisajili muda wa sekunde 10.01 mara mbili kisha akatimka kwa 10.0 kabla ya kuweka rekodi mpya ya sekunde 9.86 nchini Austria mwezi jana.

Ndiye Mkenya wa kwanza kuwahi kupata ufanisi huo na kwa pamoja na Frankie Fredericks wa Namibia, ndiye mtimkaji wa pili mwenye kasi ya juu zaidi barani Afrika baada ya Akani Simbine wa Afrika Kusini (9.84).

Japo anatazamiwa kuendeleza ubabe huo leo usiku, atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Simbine na Mmarekani Trayvon Bromell (9.77) aliyezoa nishani ya fedha Olimpiki za Tokyo.

Ferguson Rotich (1:42.54) anapigiwa upatu wa kuongoza Wakenya wenzake Cornelius Tuwei (1:43.76) na Collins Kipruto (1:43.95) kutawala mbio za 800m kwa wanaume.

Kivumbi hicho kimevutia pia Wabelgiji watano na Mouad Zahati wa Morocco (1:44.78).Mary Moraa atakuwa mwakilishi wa Kenya katika mbio hizo za mizunguko miwili kwa upande wa wanawake.

Atatoana kijasho na Natoya Goule wa Jamaica (1:56.15), Habitam Alemu (1:56.71) na Mganda Halima Nakaayi (1:58.03).

Mbio za 5,000m wanawake zitanogeshwa na Wakenya sita wakiwemo Beatrice Chebet (14:34.55), Eva Cherono (14:40.25) na bingwa mara mbili wa dunia Hellen Obiri (14:18.37). Wengine ni Margaret Chelimo (14:28.24), Lilian Kasait (14:36.05) na Daisy Cherotich (15:26.00).

Ingawa Wakenya wanapigiwa upatu wa kutamalaki mbio hizo za mizunguko 12 na nusu, watatolewa kamasi na Francine Niyonsoba wa Burundi (14:54.38) na Waethiopia Letesenbet Gidey (14:06.62), Ejgayehu Taye (14:14.09) na Fantu Worku (14:26.80).

Abel Kipsang (3:29.51), Charles Simotwo (3:30.30) na Boaz Kiprugut (3:35.26) watakuwa tegemeo la Kenya katika kivumbi cha 1,500m wanaume ambacho pia kimemvutia Mwethiopia Samuel Tefera (3:30.71).

You can share this post!

Shule zakosa maji ya kupikia watoto

Maafisa sita wa polisi wakataa mawakili sita walioteuliwa...