• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Maafisa waharibu lita 80 za chang’aa, wauzaji wakwepa mtego

Maafisa waharibu lita 80 za chang’aa, wauzaji wakwepa mtego

NA SAMMY KIMATU

MAAFISA wamefanya msako mkali na kunasa vileo haramu katika mitaa ya mabanda ya Mukuru-Commercial na Mukuru-Mariguini, tarafa ya South B.

Operesheni hiyo ya Alhamisi imeongozwa na chifu wa lokesheni ya Mukuru-Nyayo Bw Paul Mulinge akishirikiana na machifu wenzake, manaibu wao, polisi na kamati za Nyumba Kumi.

Naibu Kamishna wa Starehe Bw John Kisang alisema misako zaidi inaendelea na kwamba wanalenga kufaulu kwa asilimia 78 katika kila operesheni.

“Ni misako inayofanywa kila mwezi katika maeneo yanayokisiwa kuwa sugu kwa kuuza na kutengeneza vinywaji haramu,” Bw Kisang akasema.

Jumla ya lita 80 za pombe haramu ya chang’aa zilinaswa na kuharibiwa na maafisa hao.

Hata hivyo, hakuna mshukiwa aliyekamatwa katika tukio hilo duru zikieleza kwamba wahusika walikuwa wamepashwa habari kabla ya msako kufanywa ndiposa wakafanikiwa kutoroka.

Katika kila nyumba kulikopatikana pombe hiyo, maafisa walihakikisha wameng’oa mlango wa nyumba na kuubeba.

Mkuu wa tarafa ya South B, Bw Solomon Muraguri aliambia Taifa Leo kwamba milango yote itakusanywa na kisha kubebwa na kupelekwa katika baadhi ya shule kutumika kama kuni.

“Baada ya kung’oa milango kwenye vileo haramu, tunaibeba na kuipeleka katika shule za umma kutumika kama kuni,” Bw Muraguri akasema.

Akaongeza: “Vilevile, baada ya wamiliki wa nyumba kujua milango ya nyumba zao haipo kutokana na misako yetu, bila shaka watavuruga na kumfukuza aliyekodisha nyumba yake.”

Hatua hiyo, alisema itasaidia wamiliki wa nyumba kuwasaidia katika vita dhidi ya pombe haramu.

  • Tags

You can share this post!

Kocha wa zamani wa PSG kufunza Olunga klabuni Al-Duhail

Serikali yakatiza mkataba na madaktari wa Cuba

T L