• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Mackenzie sasa alegeza kamba kuhusu kuhojiwa na Seneti

Mackenzie sasa alegeza kamba kuhusu kuhojiwa na Seneti

NA BRIAN OCHARO

MSHUKIWA wa kuongoza dhehebu lililosababisha vifo vya waumini msituni Shakahola, Kaunti ya Kilifi, Bw Paul Mackenzie, amelegeza msimamo wake kuhusu hitaji la kufika mbele ya kamati ya seneti inayochunguza chimbuko la vifo hivyo.

Wiki iliyopita, kupitia kwa wakili wake Wycliffe Makasembo, mshukiwa huyo aliye kizuizini alikuwa amesema mahakamani kwamba hataenda mbele ya kamati hiyo hadi kesi yake ipige hatua.

Hata hivyo, jana aliiomba kamati ya Seneti iahirishe vikao vya kumhoji vilivyopangiwa kufanyika leo ili apate muda wa kujiandaa.

Kupitia kwa wakili wake, Bw Wycliffe Makasembo, alilalamika kwamba tarehe iliyopendekezwa na seneti ya Oktoba 17, haikumpa muda wa kujiandaa na hivyo basi anahisi hatatendewa haki.

‘Tafadhali pendekeza tarehe nyingine, tuseme baada ya mwezi mmoja hivi ili kumwezesha mteja wetu awasiliane nasi na kufanya uamuzi sahihi na kujiandaa vyema kujibu maswali. Vinginevyo kwa nia na madhumuni yote, Oktoba 17 ni tarehe karibu sana,” Bw Makasembo alisema katika barua yake kwa Seneti.

Kulingana na wakili huyo, mteja wake aliitwa mara ya kwanza Oktoba 13, lakini barua hiyo iliwafikia siku mbili baadaye.

Wiki iliyopita, wakati wa kikao cha Mahakama huko Shanzu, wakili huyo alimweleza Hakimu Mwandamizi Mkuu Yussuf Shikanda kwamba hayuko tayari kujiwasilisha mbele ya kamati yoyote hadi atakapomalizana na kesi ya jinai inayoendelea mahakamani hivi sasa.

‘Ninataka kumfahamisha Seneta Danson Mungatana kwamba hatutafika mbele ya Kamati yoyote ya Seneti hadi tutakapomaliza kesi hii ya uhalifu. Asipoteze wakati wake bure,’ akasema Bw Makasembo.

Kamati hiyo ilitishia kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wasimamizi wa magereza endapo hawangempeleka Bw Mackenzie mbele yao walivyoagizwa.

Bw Mackenzie na washukiwa wenzake 28 wanazuiliwa huku uchunguzi kuhusu kuhusika kwao katika mkasa wa Shakahola ambao uliacha mamia ya wafuasi wa kanisa la Good News International wakiwa wamekufa na wengine kukosa lishe bora ukiendelea.

Serikali imeomba kuongezewa muda hadi miezi sita ili kuwazuilia huku uchunguzi ukiendelea.

Muda huu wa nyongeza utatumika kutekeleza michakato muhimu ya kisayansi ya kutambua miili 429 iliyofukuliwa kutoka msitu wa Shakahola.

Imebainika kuwa takriban miili 360 iliharibika vibaya na kuathiri ubora na wingi wa sampuli za DNA zinazohitajika kutoa majibu kamili ya kutambua walioangamiza katika msitu wa Shakahola.

  • Tags

You can share this post!

Israeli yakanusha kusitisha mashambulio Ukanda wa Gaza

Shule ya Amabuko yatuliza wazazi baada ya wanafunzi 120...

T L