• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Israeli yakanusha kusitisha mashambulio Ukanda wa Gaza

Israeli yakanusha kusitisha mashambulio Ukanda wa Gaza

JERUSALEM, ISRAELI
NA MASHIRIKA
ISRAELI hapo jana ilisema kwamba hakuna mwafaka wowote uliofikiwa kuhusu kusitishwa kwa mashambulio kusini mwa ukanda wa Gaza.
Hili linafuatia taarifa zilizotolewa na vikosi vya usalama vya Misri, kuwa kuna mwafaka uliofikiwa kuhusu usitishaji wa mashambulio yanayoendelea, ili kuruhusu raia wa kigeni waliokwama Palestina kuondoka.
Vikosi hivyo pia vilisema mwafaka huo unalenga kutoa nafasi kwa mashirika ya kimisaada kuwafikia watu walioathiriwa na mashambulio yanayoendelezwa na Israeli.
Hapo jana, wakazi wa Gaza walisema kuwa Israeli iliendeleza mashambulio yake ya angani Jumapili usiku, huku wakiyataja kuwa mabaya zaidi tangu mapigano baina ya wanamgambo wa Hamas na vikosi vya Israeli kuanza, siku 10 zilizopita.
Kutokana na mgogoro wa kibinadamu ambao umeikumba Gaza, vikosi vya usalama vya Misri vilisema Israeli ilikuwa imekubali kusitisha mashambulio yake kwa muda kusini mwa Gaza. Vikosi hivyo vilisema kuwa kituo cha mpakani cha Rafah, kinachosimamiwa na Misri, kilitarajiwa kufunguliwa upya, ili kuruhusu raia wa kigeni wenye paspoti kuondoka.
Hata hivyo, afisi ya Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, ilisema kwenye taarifa: “Hakuna mwafaka wowote kuhusu usitishaji wa mashambulio Gaza ili kuwaruhusu raia wa kigeni kuondoka.”
 Jeshi la Israeli na ubalozi wa Amerika nchini Israeli hazikutoa taarifa yoyote. Maafisa na viongozi wa Hamas pia hawakuthibitisha kuhusu uwepo wa mwafaka wowote wa kusitisha mashambulio.
Hapo jana, hali ya taharuki iliendelea kushuhudiwa katika kivukio cha mpakani cha Rafah, kwani ndicho cha pekee ambacho hakijadhibitiwa na Israeli. Hali ya kibinadamu iliripotiwa kuwa mbaya katika eneo nzima la Gaza, kwani hifadhi ya chakula inaendelea kupungua.
Juhudi za kidiplomasia kuruhusu eneo hilo kupokea misaada kutoka kwa wahisani na mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada bado hazijafua dafu, tangu Israeli kuanza mashambulio makali dhidi yake Oktoba 7.
Wanamgambo wa Hamas walifaulu kuwaua raia 1,300 wa Israeli, kwenye shambulio la ghafla walilofanya nchini humo.
Jana, maafisa wa utawala wa Palestina walisema kuwa karibu Wapalestina 2,750 wameuawa kutokana na mashambulio ya Israeli. Kati ya wale waliofariki, robo yao inakisiwa kuwa watoto, huku idadi ya watu waliojeruhiwa ikifikia karibu 10,000.
Watu wengine 1,000 hawajulikani waliko, huku baadhi yao wakiaminika kufunikwa na vifusi vya majengo yaliyobomoka.
Misaada mingi kutoka mataifa kadhaa imekwama nchini Misri, nchi hizo zikisema zinangoja mashambulio hayo kusitishwa ili kuwapelekea misaada waathiriwa wa mashambulio hayo.
Misri ilisema mashambulio hayo yamekifanya kivukio cha Rafah kutopitika hata kidogo. Amerika imewaambia raia wake walio Gaza kukaribia kivukio hicho ili waweze kuondoka. Ilisema inakisia idadi ya raia wake Gaza kuwa kati ya 500 na 600.
  • Tags

You can share this post!

Hofu huku idadi ya wanaume wanaokosa nguvu za kiume...

Mackenzie sasa alegeza kamba kuhusu kuhojiwa na Seneti

T L