• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Mahangaiko ya Nakuru kuwa katika ‘lockdown’

Mahangaiko ya Nakuru kuwa katika ‘lockdown’

Na RICHARD MAOSI

MARUFUKU ya ama kutoka au kuingia katika Kaunti ya Nakuru yamekabiliwa na changamoto katika mpaka wa Nakuru-Nyandarua, waendeshaji bodaboda wakianza kusaidia wapitanjia kutumia njia za mkato.

Ukiukaji huu wa sheria unalemaza bidii ya polisi kwenye kizuizi cha Dundori katika Kaunti ya Nakuru. Hili linajiri huku visa vya corona vikiendelea kuongezeka. Jumapili kaunti hiyo iliandikisha visa 34 na vifo viwili vinavyofikisha jumla ya vifo 183 Nakuru.

Operesheni katika barabara kuu ya Ol-Kalou kuelekea Ol-Joro-Orok, inaendelea huku magari yanayotoa huduma muhimu ya kusafirisha vyakula yakiruhusiwa kupita.

Wenzao wasiotoa huduma muhimu wakishauriwa kuendelea kukaa nyumbani , katika hatua ya kusaidia kudhibiti corona.

Aidha wamiliki wa matatu, na wasafiri walilazimika kushinda majumbani kwao hii ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya serikali kuu kwa ushirikiano na kaunti kuzuia msambao wa corona ndani na nje ya Nakuru.

Taifa Leo iligundua kuwa baadhi ya wasafiri bado walikuwa wakitumia vichochoro ili kuhepa mkono wa sheria; wengi wao wakisema agizo la Rais Uhuru Kenyatta lilikuwa la ghafla mno.

Nao wafanyabiashara walieleza jinsi ambavyo hatua hiyo imeyumbisha biashara. Mmoja wao akiwa ni Margret Waithera ambaye anasema alikuwa akijiandaa kupeleka watoto wake mashambani kaunti ya Laikipia watakapomaliza mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) Aprili 22, 2021. Anasema kwa sasa biashara yake imeshuka, kwa sababu awali alikuwa akiuza viazi kwa kaunti mbili ila hivi sasa kizuizi kimemfungia Nakuru.

“Tunaomba Rais wetu mpendwa kutoa muda zaidi kwa wazazi kujiandaa badala ya kufunga mipaka ghafla,” alisema Bi Waithera.

Kwa upande mwingine James Mwangi ambaye ni mfanyabiashara katika eneo la Dundori anasema kuwa biashara yake ya kuuza saruji na vifaa vya ujenzi itaporomoka endapo hataorodheshwa kama mtoaji wa huduma muhimu.

“Mara nyingi nimekuwa nikifanya biashara hadi Lanet, lakini kuanzia leo asubuhi  niliamua kufunga duka baada ya malori yangu yote ya uchukuzi kuzuiliwa na polisi,” akasema.

You can share this post!

Aliyenaswa kwa video akimtesa mshukiwa wa wizi Ajab Mills...

Cha kufanya ili kuondoa maumivu ya miguu baada ya mazoezi