• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Majina ya Ruto na Kindiki yasababisha vikao vya Shakahola kuahirishwa

Majina ya Ruto na Kindiki yasababisha vikao vya Shakahola kuahirishwa

NA RICHARD MUNGUTI

KIKAO cha mahojiano kati ya Pasta Ezekiel Odero wa Kanisa la New Life Prayer Centre & Church na wanachama wa kamati maalum ya Seneti kilisitishwa  ghafla majina ya Rais William Ruto na Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki yalipotajwa.

Hii ni baada ya Pasta Odero kudai Kamishna wa Kaunti ya Kilifi Joseph Biwott alizima mitambo yake ya krusedi kwa kufuata maagizo ya wakuu hawa wa serikali.

Ufichuzi huu ulizua tumbojoto Pasta Odero aliposema “niliitwa na Biwott na akanieleza kwamba amepokea simu kutoka kwa Rais Ruto na Prof Kindiki kuniagiza nizime mitambo ya Injili.”

Pasta Odero aliekeza kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Tana River Danson Muungatana ilibidi asitishe krusedi kufuatia maagizo hayo ya Rais Ruto na Prof Kindiki.

Ni wakati huo huo Seneta wa Migori  Eddy Oketchi aliomba Pasta Odero akubaliwe kutoboa siri ndipo kamati hiyo ibaini baadhi ya maafisa serikali wanaotumia mamlaka yao vibaya kumzima muhubiri huyu kueneza habari njema.

“Naomba Pasta Odero akubaliwe kuwataja wote waliomzima asieneze injili ndipo ripoti tutakayoandaa kumpelekea Rais Ruto iwe imekamilika,” Bw Oketch alisema.

Naye  Seneta wa Nandi Samson Cherargei aliitaka kamati hiyo imshurutishe Pasta Odero kuondoa madai dhidi ya Rais Ruto akisema hapasi kuruhusiwa kutaja ovyo ovyo jina la Rais.

“Kwa mujibu wa Katiba Rais anatakiwa kutoa maagizo kwa kuandika barua na wala sio kupiga simu. Ikiwa Pasta Odero hana barua kuonyesha Rais Ruto alimwamuru Bw Biwott asitishe krusedi basi pasta huyu anatakiwa kuondoka matamshi hayo,”alisema Bw Cherargei.

Bw Cherargei alimtaka naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Bi Shakil Abdallah atoe mwelekeo.

Naye Seneta wa Kisii Richard Onyonka alisema Pasta Odero hapasi kuzuiliwa kuwataja wote waliohusika kuzima uenezaji injili.

Kamati hiyo ilisema vikao vyake ni spesheli na zinaweza kupokea ushahidi wowote ule.

Akiendelea kuhojiwa Pasta Odero alijitenga na Pasta Paul Mackenzie kwa kusema “nilimuona tu kwa televisheni ya KBC akidaiwa amehusika na mauaji ya halaiki ya watu Shakahola.”

Akasema Pasta Odero: “Naomba maafisa wa DCI na kamati hii mtembelee kanisa langu Mavueni na mtembee kila mahali, mkipata kaburi moja hata kama ni yap aka aliyekufa msisite kunichukulia hatua. Sijawahi husika na mambo ya Shakahola iliyo umbali wa kilomita 200 kutoka Mavueni.”

Aliendelea na kusema,“Hakuna mtu hata mmoja aliyekufa katika kanisa langu na wala sienezi injili yenye itikadi kali inayoweza kufanya watu wajinyime chakula,” alisema Pasta Odero.

Alisema amejenga hoteli mbili katika uwanja wa kanisa lake na baada ya kila ibada watu huenda kujipatia chakula na kurudi tena kwa ibada.

Pasta huyo aliioomba kamati hiyo izuru kanisa lake kujionea kile kinachoendelea badala ya kutegemea habari za mitandao.

Alisema anawasaidia kuwasomesha wanafunzi zaidi ya 200 kutoka familia maskini na kwamba amejenga kanisa kubwa inayohudhuriwa na waumini 45,000 kila ibada.

Alisema hapokei ufadhili wowote kutoka nje ila anatumia sadaka na fungu la kumi linalotolewa na waumini.

“Sihubiri injili ya kuwanyanyasa washirika. Washirika hutoa sadaka waliyo nayo,” Pst Odero alieleza kamati hiyo.

Awali Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) Amin Mohammed alijhojiwa faraghani baada ya kueleza kamati hiyo ushahidi aliotoa utaghusia masuala ya usalama wa kitaifa.

Pasta Odero aliyetoa ushahidi kwa zaidi ya masaa manne alisema hana uhusiano wowote na mhubiri Mackenzie anayezuiliwa katika gereza la Shimo la Tewa Mombasa anayehusishwa na mahubiri potovu yaliyochangia vifo vya watu msituni Shakahola.

Pasta Odero ambaye Ijumaa asubuhi amefika mbele ya Kamati Maalum ya Seneti Inayochunguza Shughuli za Kidini ameambia wanahabari nje ya Majengo ya Bunge kwamba “Kanisa langu linajitegemea na la Mackenzie pia linajitegemea.”

Pasta Odero ambaye tangu Aprili 2023 amekuwa akimulikwa huku umma ukifuatilia matukio na shughuli za kanisa lake lenye ukwasi mkubwa. Mbali na Kanisa, Pasta Odero ameanzisha miradi mingine ya shule za msingi na za upili pamoja na hoteli za kifahari katike eneo la Mavueni, Kaunti ya Kilifi.

“Mimi ni raia anayetii sheria na nimejileta mbele ya kamati maalum ya Seneti kujibu maswali nitakayoelekezewa,” amesema Pasta Odero aliyekuwa amevaa vazi lake jeupe.

Akaongeza:” Haya yote ni kwa sababu ninaendeleza Neno na kuzungumzia masuala yanayohusu Yesu Kristo na mafundisho mazuri. Hakuna kitu kama hiki kilichowahi kufanyika hapo kabla lakini nitashinda.”

Pasta huyo alikuwa ameambatana na Pasta Pius Muiru wa Kuna Nuru Gizani.

Pasta Muiru, ambaye ni mlezi wa kiroho wa Pasta Odero amesema wataweka mambo yote wazi kwa Seneti.

“Dunia itajua ukweli kuhusu Pasta Odero na injili anayoendeleza,” Pasta Muiru akasema.

Mawakili wa Pastor Odero waliofika kikaoni naye ni Samson Nyaberi, Shadrack Wambui, Danstan Omari, na Cliff Ombeta.

Mawakili hao wamesema kuna kesi nyingi ambazo hazijaamuliwa na ambazo zinamkabili mteja wao na injili anayoendeleza.

“Pasta Odero ni safi na mweupe kama mavazi yake,” akasema wakili Omari.

Naye wakili Nyaberi amesema akaunti 28 za Pasta Odero zilizokuwa zimefungwa zimefunguliwa baada ya Mahakama Kuu kuingilia kati.

Wakili Ombeta kwa upande wake amesema kuna tofauti kubwa kati ya Pasta Odero na mhubiri Mackenzie.

“Kila mtu anajua huko Shakahola zaidi ya miili 400 ilipatikana kwenye makaburi katika shamba kubwa.”

Wakili Omari amesema watasema yote muhimu kwenye kamati hiyo maalum ambayo itataka kusikia maoni kutoka kwa Pasta Odero na namna ya kudhibiti makanisa.

  • Tags

You can share this post!

Mwanahabari wa NMG anyakua tuzo ya Kani ya Maneno ya 2023...

Raila Odinga alivyofurushwa Turkana, MCA akimchemkia kwa...

T L