• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Mwanahabari wa NMG anyakua tuzo ya Kani ya Maneno ya 2023 ya Global Energy

Mwanahabari wa NMG anyakua tuzo ya Kani ya Maneno ya 2023 ya Global Energy

NA LEON LIDIGU

MWANAHABARI wa Nation Media Group (NMG) Pauline Ongaji ameelezea furaha yake baada ya kunyakua tuzo ya kategoria ya kimataifa kutoka kwa Global Energy.

Tuzo hiyo ya Kani ya Maneno ya Mwaka 2023 ilitolewa mnamo Ijumaa, Oktoba 13, 2023, ambapo Shirley Acosta Licero wa Mónica Vargas León, IPSE (Colombia) aliibuka wa pili huku Amit Baijnath Garg wa The Desert Trail (India) akifunga tatu-bora.

Jumla ya washiriki 262 kutoka Urusi na 23 kutoka mataifa ya kigeni walituma kazi zao kutathminiwa kuwania tuzo ya Kani ya Maneno.

Washindi waliamuliwa na paneli ya majaji waliojumuisha wakuu wa vituo vya runinga, majarida ya kibiashara na mashirika ya habari.

Rais wa Global Energy Sergey Brilev, alihudhuria hafla ya kuwatuza washindi.

Pauline amesema tuzo hiyo inamshajiisha kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kubadilisha maisha ya wengi katika jamii na duniani kwa ujumla.

“Tuzo hii nimeipokea kwa mikono miwili na ninamshukuru Mwenyezi Mungu,” amesema Pauline akihojiwa na Taifa Leo mapema Jumamosi.

Mhariri Mkuu Msimamizi wa NMG Pamella Sittoni amemtunuka Pauline sifa, akimtaja kuwa ni mwanahabari wa sayansi anayejizatiti kila siku kuibuka na habari na makala yanayolenga kubadilisha maisha ya wengi katika jamii.

“Pauline ameletea NMG sifa kwa kuzoa tuzo hii. Uandishi wake wa sayansi ambapo amejikita sana kwa afya na mabadiliko ya tabianchi, umemkweza na ndipo akaamua kufanya utafiti wa shahada yake ya uzamili akiegemea kwa mbinu za kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” akasema Bi Sittoni.

Naye mhariri wa jarida la Saturday Magazine – lililochapisha makala yake yaliyoteuliwa kwa tuzo – Bi Phyllis Nyambura amesema Pauline ni mwandishi anayezamia kazi yake barabara kwa lengo la kuhakikisha kazi inakuwa na athari inayoonekana.

“Nina furaha kwa sababu tukisuka makala hayo ya kuwaangazia wanawake wanaopiga hatua katika sekta ya nishati jadidifu, ilitubidi tuangazie namna ambavyo tungefanya wasomaji waelewe kazi hiyo upesi na iwe ni ya kuwaburudisha,” akasema Bi Nyambura.

Kwa sasa Pauline, ambaye anapongeza mhariri wake, familia na mwanahabari mwenzake kutoka nchini Afrika Kusini Melody Chironda kwa kumtia moyo kuangazia wanawake wanaojizatiti na kuzamia katika sekta ya nishati safi, anasema ana hamu ya kuwa mmojawapo wa wanahabari watakaohudhuria na kuripoti matukio ya Kongamano la COP28 linalotarajiwa kufanyika jijini Dubai mnamo Novemba 2023.

Tuzo ya Kani ya Maneno ya Global Energy imekuwepo tangu mwaka 2003.

  • Tags

You can share this post!

Martial wa Man United atema visura wawili, aoga na kurudi...

Majina ya Ruto na Kindiki yasababisha vikao vya Shakahola...

T L