• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
Makao Makuu ya Katoliki Vatican hatarini kufilisika

Makao Makuu ya Katoliki Vatican hatarini kufilisika

Na VALENTINE OBARA

MAKAO makuu ya Kanisa Katoliki ulimwenguni yaliyoko Vatican, yametoa wito kwa waumini na wafadhili kuchangia ili kuepushia kanisa uwezekano wa kufilisika.

Kanisa hilo linaloongozwa na Papa Francis limekiri kukumbwa na matatizo ya kifedha tangu mwaka uliopita kwa sababu ya janga la virusi vya corona, hali iliyofanya pia hazina ya pesa zake za matumizi ya dharura kuanza kukauka.

Waziri wa masuala ya uchumi wa Vatican, Kasisi Juan Antonio Guerrero Alves, alieleza kuwa changamoto imetokea kwa sababu taifa hilo ni la kipekee ambalo hutegemea sana ufadhili badala ya mikopo jinsi ilivyo katika mataifa mengine ulimwenguni.

“Mwaka huu mapato yamepungua. Kama tungekuwa shirika la kibiashara au lisilo la kiserikali (NGO) tungepunguza huduma zetu na idadi ya wafanyakazi. Kama tungekuwa taifa linalofanana na mengine, tungechukua mikopo zaidi na kuweka mikakati mingine ya kifedha. Lakini kwetu sisi, tusipopata ufadhili, itabidi tuendelee kutumia pesa kutoka kwa hazina ya dharura,” akasema.

Alisema hayo kwenye mahojiano yaliyochapishwa na tovuti rasmi ya Vatican mnamo Ijumaa.

Alves alisema ijapokuwa matumizi ya fedha yalipungua kwa shughuli za kawaida kama vile kuandaa mikutano na safari mbalimbali, kuliibuka shughuli nyingine wakati wa janga la corona zilizohitaji matumizi zaidi ya fedha.

Alitoa mfano wa utoaji misaada kwa jamii kupitia kwa mashirika ya Kikatoliki ulimwenguni hasa katika mataifa ambayo yalikuwa na idadi kubwa ya watu ambao walipoteza ajira na biashara wakati janga la corona lilipotokea.

Hata hivyo, alijaribu kuwaondolea waumini wasiwasi kwa kusema hali inayokumba Vatican si tofauti na inayoshuhudiwa katika nchi nyingine nyingi kwa sababu ya janga la corona.

Kulingana na Alves, kuna matumaini hali ya kawaida itarudi hivi karibuni na uchumi utaanza kufufuka.

“Mapato yanayotokana na ukodishaji wa vyumba na shughuli nyingine za kiuchumi yataanza kupatikana wakati uchumi utarudi hali ya kawaida. Makavazi (yetu) yataanza kufunguliwa bila vikwazo na watalii watarudi kwa wingi. Kilicho muhimu ni kutumia vyema pesa tulizo nazo kwa sasa na tuwe na uwazi kuwapa waumini habari zinazowatuliza akili kuhusu sadaka wanazotoa,” akasema.

Alisisitiza kuwa hitaji muhimu la Vatican ni kuwa na kiwango cha kutosha cha fedha cha kuendeleza shughuli za kimishenari za Kanisa Katoliki zinazosimamiwa na Papa Francis.

You can share this post!

Wanaomezea ‘tosha’ ya Uhuru

Raila aondoka hospitalini, kuendelea kujitenga nyumbani