• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 2:53 PM
Marudio ya uchaguzi wa viongozi wa GTMA yafanyika kwa amani na utulivu

Marudio ya uchaguzi wa viongozi wa GTMA yafanyika kwa amani na utulivu

Na SAMMY WAWERU

HATIMAYE uchaguzi wa viongozi wa muungano wa wahudumu wa tuktuk eneo la Githurai 45 (GTMA), kiungani mwa jiji la Nairobi, umefanyika.

Uchaguzi huo umefanyika miezi mitatu baada ya uliofanyika mnamo Novemba 13, 2020 kufutiliwa mbali kwa madai ya kukumbwa na udanganyifu wa kura.

Baadhi ya wagombea walipinga matokeo, wakihoji kwamba zoezi hilo halikuwa la huru, haki na uwazi.

Waliwasilisha malalamishi kwa Afisi ya Masuala ya Jinsia, Utamaduni na Huduma za Kijamii (SCDO), Kaunti Ndogo ya Ruiru,na iliyosimamia shughuli hiyo.

Ushahidi uliotolewa uliishawishi SCDO kuharamisha matokeo.

Muungano huo umejumuisha tuktuk na magari madogo aina ya maruti, kijumla yakikadiriwa kuwa zaidi ya 300.

Aidha, marudio ya uchaguzi huo yalihusisha wamiliki pekee, ambapo wapiga kura 114 ndio walijitokeza.

Shughuli hiyo ilianza mwendo wa saa nne asubuhi, chini ya usimamizi wa Bi Ann Kamau, afisa kutoka SCDO na ambaye pia aliandamana na maafisa kadha.

Lilifanyika katika ukumbi wa mikutano ulioko katika afisi ya D.O Githurai, Ruiru, chini ya ulinzi wa maafisa wawili wa polisi.

Kinyume na ilivyotarajiwa fujo na vurugu kuzuka, marudio hayo yalisheheni amani na mpangilio wa aina yake.

“Nimefurahishwa na jinsi wapiga kura walishiriki zoezi zima, kwa amani na utulivu. Mpangilio wa maandalizi ulikuwa bora,” akaridhia Bi Kamau.

Nyadhifa zilizowaniwa ni pamoja na nafasi ya mwenyekiti wa GTMA, naibu mwenyekiti, katibu mkuu, karani, naibu karani, mweka hazina na kiongozi wa nidhamu.

Maafisa kutoka Afisi ya Masuala ya Jinsia, Utamaduni na Huduma za Kijamii (SCDO), Kaunti Ndogo ya Ruiru wakisimamia uchaguzi wa viongozi wa muungano wa wahudumu wa tuktuk na maruti eneo la Githurai 45 (GTMA). Picha/ Sammy Waweru

Kiti cha mwenyekiti kilikuwa na mwaniaji mmoja pekee, na Bw Laban Gitonga alichaguliwa bila pingamizi.

Aidha, kiti cha naibu mwenyekiti pia kilikuwa na mgombea mmoja, kikitwaliwa na Bw Peter Kinuthia.

Huduma za usafiri na uchukuzi eneo la Githurai kupitia GTMA zimebuni nafasi za ajira kwa vijana wengi, kuanzia madereva walioajiriwa hadi wafanyakazi katika steji.

Ni kati ya sekta ambazo zinasaidia uchumi Kaunti ya Kiambu kukua na kuimarika kwa kasi.

Kiti cha mweka hazina na ambacho kimejukumika kukusanya pesa za utoaji huduma kilikuwa chenye ushindani mkali.

Bw Bernard Gatugi aliibuka kidedea kwa kuzoa kura 66, akifuatwa na mshindani wake, Bw Peter Mainga aliyepata 46.

Wadhifa mwingine muhimu katika GTMA ni katibu mkuu, na Mark Miano aliibuka mshindi kwa kupata kura 74, huku mpinzani wake Elias Ngugi akizoa kura 31.

Uchaguzi huo ulitajwa kama uliokuwa huru na wenye uwazi tangu tuktuk zijiri Githurai mwaka wa 2014.

Aidha, upigaji kura ulikuwa wa mfumo wa siri.

Kila aliyeshiriki, majina yake yalikaguliwa katika sajili ya wamiliki, nambari zake za kitambulisho cha kitaifa na za simu pia zinajumuishwa, kisha anakabidhiwa kura zenye majina ya wagombea.

Kura hizo zilikuwa na nambari. Baada ya kuchagua, kila mpiga kura alipakwa rangi kwenye kidole ili kuepuka upigaji kura mara mbili.

Bw Laban Gitonga, mwenyekiti mteule, alihimiza wawekezaji katika sekta hiyo kushirikiano na viongozi waliochaguliwa ili kuimarisha biashara hiyo.

“Ninawaomba tushirikiane, tuendeleze hii biashara itufae na ifae madereva wetu na wafanyakazi wengine,” akasema.

Gitonga amemrithi mtangulizi wake, Bw Peter Kinyua na ambaye hakuwa debeni kutetea kuhifadhi nafasi yake.

Maandalizi ya uchaguzi huo yalifanikishwa na afisi ya muda iliyoteuliwa na kamati ya ushauri, baada ya kipindi cha viongozi waliokuwepo kukamilika mwishoni mwa 2020.

SCDO imehimiza muungano huo kukumbatia uwekaji akiba ili kuboresha utendakazi.

Kwenye hotuba yake, mweka hazina mteule, Bernard Gatugi aliahidi kuweka mikakati kabambe wanachama wa GTMA kukumbatia suala la uwekaji akiba.

“Si ajabu tukijipanga tufungue kituo cha mafuta, duka la vipuri vya tuktuk, kati ya maendeleo mengine,” Bw Gatugi akasema, akilalamikia mamilioni ya pesa kufujwa na afisi za awali.

Kwa upande wake mbunge wa Ruiru, Bw Simon King’ara aliahidi kushirikiana na GTMA, na pia kusaidia kuimarisha usalama katika sekta hiyo.

  • Tags

You can share this post!

FATAKI: Ikiwa wewe bahili wa mali na moyo, basi mapenzi...

Sagan Tosu anayochezea Mkenya Ismael Dunga yasaga Shonan...