• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:50 AM
Sagan Tosu anayochezea Mkenya Ismael Dunga yasaga Shonan Ligi Kuu ya Japan iking’oa nanga

Sagan Tosu anayochezea Mkenya Ismael Dunga yasaga Shonan Ligi Kuu ya Japan iking’oa nanga

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Sagan Tosu ilianza Ligi Kuu ya Japan (J1 League) kwa kulemea wenyeji Shonan Bellmare 1-0 Jumamosi.

Mkenya Ismael Dunga, ambaye Februari 24 alisherehekea kugonga umri wa miaka 28, hakushiriki mchuano huo.

Mshambuliaji huyo wa kati bado hajaingia Japan tangu asainiwe kutoka Vllaznia nchini Albania mwezi Januari kutokana na marufuku dhidi ya usafiri nchini Japan ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. Marufuku hiyo, ambayo imesababisha kusimamishwa kwa shughuli ya utoaji wa vibali vya kusafiria (visa), inatarajiwa kukamilika Machi 7. Hata hivyo, ripoti nchini Japan zinasema kuwa huenda wageni bado watahitajika kuingia karantini ya siku 14 marufuku hiyo ikiondolewa, kabla ya kujiunga na wenzao.

Hapo Jumamosi, Sagan ilichapa Shonan Bellmare 1-0 kupitia penalti kutoka kwa Daichi Hayashi dakika ya 80.

Katika michuano mingine, waajiri wa zamani wa mshambuliaji Mkenya Michael Olunga, Kashiwa Reysol walifungua msimu kwa kupepetwa 2-0 na Cerezo Osaka. Hokkaido Consadole Sapporo walizoa ushindi mkubwa wa siku ya kwanza walipokanyaga Yokohama FC 5-1. Katika mechi nyingine, Urawa Red Diamond ilitoka 1-1 dhidi ya FC Tokyo, Oita Trinita na Tokushima Vortis zikagawana alama katika sare ya 1-1 nayo Kashima Antlers ikakubali kichapo cha magoli 3-1 kutoka kwa Shimizu S-Pulse. Vissel Kobe ilizidia Gamba Osaka ujanja 1-0.

You can share this post!

Marudio ya uchaguzi wa viongozi wa GTMA yafanyika kwa amani...

Kandie, Chelangat waonyesha wenzao kivumbi mbio za mita...