• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Marudio ya uchaguzi wa viongozi wa muungano wa tuktuk na maruti Githurai kufanyika Februari 2021

Marudio ya uchaguzi wa viongozi wa muungano wa tuktuk na maruti Githurai kufanyika Februari 2021

Na SAMMY WAWERU

MARUDIO ya uchaguzi wa muungano wa wahudumu wa tuktuk na maruti Githurai 45 (GTMA) yameratibiwa kufanyika mnamo Februari 25, 2021.

Kamati maalum ya muda iliyobuniwa kusimamia shughuli za utendakazi wa wahudumu hao baada ya afisi iliyokuwepo kuondolewa, imetoa notisi ikiwataka wagombea wa nyadhifa zitakazowaniwa kuendesha kampeni kwa amani na utulivu.

“Marudio ya uchaguzi uliofutiliwa mbali utafanyika Februari 25, 2021, watakaowania nyadhifa tafadhalini endesheni kampeni kwa njia ya amani na utulivu,” inaeleza notisi hiyo.

Uchaguzi wa GTMA uliofanyika mwishoni mwa mwaka uliopita, Novemba 13, 2020 ulifutiliwa mbali baada ya baadhi ya wagombea kulalamikia ulikumbwa na utapeli na wizi wa kura.

Ulikuwa umesimamiwa na serikali, chini ya Afisi ya Masuala ya Jinsia, Utamaduni na Huduma za Kijamii (SCDO), Kaunti ndogo ya Ruiru.

Githurai 45 ipo katika eneobunge la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Malalamishi yaliyoibuliwa na baadhi ya wagombea wakitaja zoezi zima “kama lililokosa uwazi” yaliishawishi SCDO kuuharamisha, ikiitaka GTMA kuandaa uchaguzi mwingine.

Aidha, SCDO imehimiza muungano huo kuandaa rejista ya wamiliki wote wa tuktuk na maruti.

Baadhi ya wamiliki wanapendekeza Katiba ya sasa ya GTMA kufanyiwa marekebisho kabla kushiriki uchaguzi mwingine, huku wakisisitiza viongozi ambao wamewahi kuwa afisini tangu huduma za tuktuk Githurai zianze wasiwanie tena.

Huduma za magari hayo madogo ya usafiri na uchukuzi zilijiri mtaani Githurai mwaka wa 2014. Eneo hilo lina zaidi ya tuktuk na maruti 300 na ambazo zimetajwa kuchangia kuimarika kwa uchumi, kubuni nafasi za ajira kwa vijana pamoja na kuingizia wamiliki mamilioni ya pesa.

Uchaguzi wa muungano huo 2020 ulifanyika katika ukumbi wa mikutano, ulioko katika afisi ya D.O, Githurai, chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi.

Ulikuwa na jumla ya nyadhifa tisa zilizowaniwa, chini ya usimamizi wa tume ya muda, iliyoiga nyayo za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), katika kuendesha uchaguzi.

  • Tags

You can share this post!

Wataalam waanza kusaka kiini cha corona jijini Wuhan

BI TAIFA JANUARI 29, 2021