• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Masaibu ya Sonko yazidi huku kesi zikifufuliwa

Masaibu ya Sonko yazidi huku kesi zikifufuliwa

BENSON MATHEKA na SIMON CIURI

Masaibu ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Sonko yaliendelea kuongezeka jana alipozuiliwa rumande baada ya kukanusha mashtaka mapya 12 anayodaiwa alifanya mnamo 2019.

Baada ya kukanusha mashtaka hayo, upande wa mashtaka ulisema unataka kumpeleka mahakama ya Mombasa ambako anahitajika kuhusiana na kesi nyingine ya 2001.

Sonko alifikishwa katika mahakama ya Kiambu chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa kikosi maalumu siku moja baada ya kujiwasilisha makao makuu ya Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) kufuatia malalamishi ya Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho.

Baada ya kuandikisha taarifa katika DCI wiki jana, Sonko alipomhusisha na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2017, Dkt Kibicho alisema mbunge huyo wa zamani wa Makadara atawajibika kwa tabia yake ya kuchafua majina ya watu.

Jana, polisi waliambia mahakama kwamba, Bw Sonko angali anachunguzwa kubaini mchango wake kwenye ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Akihutubia mkutano wa siasa eneo la Dagoretti mwezi jana, Bw Sonko alisema yeye na Dkt Kibicho walipanga ghasia hizo ili kupaka tope chama cha ODM, madai ambayo yalimkasirisha katibu huyo.

Wengi walitarajia kwamba aliitwa DCI kuandikisha taarifa kuhusu madai hayo lakini akashtakiwa kwa kuvamia ardhi ya kibinafsi mtaani Buruburu, kushambulia na kusababishia watu majeraha na wizi wa mabavu.

Polisi waliambia mahakama kwamba, mnamo Machi 25 2019, katika mtaa wa Buruburu, eneobunge la Kamukunji jijini Nairobi aliingia ardhi ya kampuni ya Landmark International Properties limited.

Mahakama ilifahamishwa kwamba, Sonko aliondoka ofisi yake akiandamana na vijana ambao aliwachochea kushambulia watu.

Alikabiliwa na mashtaka 12 ya kuongoza vijana hao kuwashambulia watu, kuwajeruhi na kuwanyang’anya mali yao.

Upande wa mashtaka uliomba mahakama asiachiliwe kwa dhamana ukisema kwamba, uchunguzi unaendelea na kwamba unataka kumpeleka Mombasa ambako mahakama ilitoa kibali cha kumkamata kuhusiana na kesi tofauti.

Kupitia hati ya kiapo, maafisa wa polisi walisema kwamba katika kesi hiyo, alitoweka baada ya kuachiliwa kwa dhamana mnamo 2001 na akiachiliwa kwa dhamana anaweza kuwatisha mashahidi ambao ni watu anaofahamu.

Mahakama iliambiwa Bw Sonko ana wafuasi wengi jijini Nairiobi na anaweza kuvuruga uchunguzi unaoendelea kuhusu madai mengine dhidi yake. Inasemekana Sonko haheshimu sheria ikizingatiwa kwamba amewahi kutoweka baada ya kuachiliwa kwa dhamana,” polisi walisema kwenye hati ya kiapo.

Mawakili wake, wakiongozwa na John Khaminwa waliomba aachiliwe kwa dhamana wakisema ni mtu maarufu Kenya na hawezi kutoroka.

Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kiambu Stella Atambo alikataa kumwachilia kwa dhamana ya pesa taslimu na kuagiza azuiliwe hadi Alhamisi atakapotoa uamuzi kuhusu ombi la kuachiliwa kwa dhamana.

Bw Sonko alivuliwa wadhifa wa gavana wa Nairobi mwaka jana baada ya kutofautiana na Rais Uhuru Kenyatta. Anakabiliwa na mashtaka kadhaa ya ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi yake alipokuwa gavana.

You can share this post!

Wanafunzi wafeli majaribio ya KCPE kwa wingi

Hazina za wanawake, vijana kuunganishwa