• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Masoko ya wazi yaruhusiwe katika kaunti zilizofungwa

Masoko ya wazi yaruhusiwe katika kaunti zilizofungwa

Na CHARLES WASONGA

INGAWA hatua ya serikali kuimarisha masharti ya kudhibiti maambukizi ya Covid-19 katika kaunti za eneo la Magharibi inafaa kupongezwa, yanawaumiza raia wenye mapato finyu.

Moja ya amri ambayo ningependa iondolewe au ilegezwe ni ya kufungwa kwa masoko ya wazi katika kaunti 13 za eneo hilo pana linalopakana na Ziwa Victoria.Hii ni kwa sababu wakazi wengi wa kaunti hizi za mashambani hutegemea masoko haya kujitafutia riziki ya kila siku.

Hivyo, kufungwa kwa masoko ya Kisumu, Siaya, Homa Bay, Kisii, Nyamira, Kakamega, Vihiga, Busia, Kericho, Bomet, Bungoma na Trans Nzoia ni sawa na kuwakatizia wakazi hawa chanzo cha mapato kwa kipindi cha siku 30.

Kunamaanisha kuwa wakazi, haswa ndani mashambani, hawatapata mahala pa kuuza mazao, mifugo na bidhaa nyinginezo za kuwaletea mapato wakati huu ambapo vianzo vyao vingine vya riziki vimeathiriwa na janga la Covid-19.Vianzo hivyo ni kama vile jamaa wanaofanyakazi miji mikuu ambao huwatumia pesa za matumizi; lakini sasa hawana uwezo wa kufanya hivyo sababu wengine wao wamefutwa kazi au kupunguziwa mishahara.

Hii, bila shaka, inaathiri pakubwa fedha wanazotumiwa wakazi hawa wanaoishi mashambani – wengi wakiwa katika kaunti hizo za eneo la Magharibi ambazo zimefungwa. Tayari wakazi wameanza kuhisi makali ya masharti hayo mapya ikizingatiwa kuwa kafyu sasa itaanza mapema saa moja jioni hadi saa kumi alfajiri, badala ya saa nne za usiku hadi saa kumi alfajiri ilivyo katika maeneo mengine ya nchi.

Itakuwa jambo la busara kwa serikali kufungua masoko katika kaunti husika za Magharibi ili wakazi wapate fursa ya kuchuma riziki ya siku.Masharti ambayo serikali inapaswa kuhakikisha yamedumishwa katika masoko, ni kwa wauzaji na wanunuzi kuvalia barakoa nyakati zote.Pia kunawa mikono kablaa na baada ya kukamilisha shughuli zao za biashara.

Vile vile, wafanyabiashara wasisitiziwe kwamba sharti wahakikishe wateja wao hawasongamani nyakati zote wakiwa sokoni.Muhimu zaidi ni kwamba, serikali inafaa kuimarisha mpango wa utoaji chanjo ya Covid-19, inayosababishwa na virusi vya corona, katika kaunti hizi 13 ambazo zimetajwa kama maeneo hatari ya maambukizi kwa sasa nchini.

Idadi kubwa ya dozi 350,000 ya chanjo ya AstraZeneca ambayo serikali ilipokea kutoka taifa la Denmark siku ya Jumatatu, ipelekwe katika maeneo hayo.Haswa kwa wakazi wa kaunti za Kisumu, Siaya na Homa Bay ambazo ndizo zinaandikisha idadi ya juu ya maambukizi ya corona wakati huu.

Kwa mfano, juzi wakazi wa kaunti ndogo ya Gem, katika kaunti ya Siaya waliomba serikali iwaruhusu kuendelea na biashara zao katika masoko ya wazi ili angalau wapate hela za kuwalipia watoto wao karo zao shule.

Kilio chao kina mashiko ikizingatiwa kuwa juzi Waziri wa Elimu aliwashauri walimu wakuu wa shule za upili kuwafukuze wanafunzi ambao wazazi wao hawajakamilisha kulipa karo za mwaka huu wa masomo. Kimsingi, wengi wa wazazi katika maeneo ya mashambani hupata pesa za kulipa karo kwa kuuza mifugo wao au mazao yao ya shambani katika masoko ya wazi ambayo sasa yamefungwa

  • Tags

You can share this post!

Maskwota elfu tatu wafurushwa

Heko Facebook kuzima akaunti za chuki Ethiopia