• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 7:50 AM
Heko Facebook kuzima akaunti za chuki Ethiopia

Heko Facebook kuzima akaunti za chuki Ethiopia

Na FAUSTINE NGILA

TUNAISHI enzi hatari ambapo watu walio na usemi mkubwa katika masuala ya kisiasa, wanatumia mitandao ya kijamii kama silaha dhidi ya wapinzani nyakati za uchaguzi.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Ethiopia uliofanyika Jumatatu, wanasiasa walifurika katika mtandao wa kijamii wa Facebook kuchapisha jumbe za chuki na kueneza habari feki, bila kujali athari ya vitendo vyao kwa wapigakura.Ni aibu iliyoje kwa taifa ambalo limeshuhudia vita katika eneo la Tigray kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, kuruhusu wanasiasa wake kuchochea uhasama baina ya jamii.

Mwanzo, hili ni taifa ambalo limekuwa likibana matumizi ya intaneti katika kipindi chote cha machafuko ya Tigray, na kuwafungia nje mamilioni ya Waethiopia wanaotaka kupata habari zinazowahusu wakati wa uchaguzi.

Kwa kugundua kuwa unahitaji tu kulipia tangazo la kisiasa kwenye Facebook ili lifikie watu wengi, wanasiasa wa nchi hiyo wameonekana kukosa maadili kwa kusambaza jumbe za kupotosha. Lakini naipongeza Facebook, maanake baada ya kung’amua jinsi wanasiasa watundu walikuwa mbioni kuwahadaa wapigakura, ilichukua hatua mara moja kufunga akaunti na makundi husika katika mtandao wake.

Kwa jumla, kampuni hiyo iling’oa akaunti 65, kurasa 52 na makundi 27. Pia iliondoa akaunti 32 kwenye mtandao wake mwingine wa kijamii – Instagram, ambazo zilikuwa zinapigia debe chuki na vurumai baina ya makabila.Kimsingi, kila ukurasa wa Facebook wa kisiasa ulikuwa na wafuasi zaidi ya milioni moja, huku watu zaidi ya 700,000 wakiwa wanachama wa vikundi vya uhasama.

Watu 1,700 walikuwa wafuasi wa kila akaunti ya Instagram.Inamaanisha kuwa, kwa kuzima kaunti hizi hatari Facebook imezuia machafuko zaidi wakati wa uchaguzi, ambao tayari umekumbwa na utata.Ni hatua ambayo imezuia vifo zaidi, kwa kupunguza kasi ya msambao wa habari feki, video za kuchochea fujo na picha tatanishi kwa wapigakura.

Ni wiki mbili tu baada ya Facebook kumpiga marufuku rais wa zamani wa Amerika, Donald Trump, kutumia akaunti yake kwa muda wa miaka miwili. Hii ilikuwa hatua njema ya kupunguza chuki duniani.Isiwe tu ni Ethiopia na Amerika pekee, Facebook sasa inafaa kuonekana kuwa mstari wa mbele katika kila nchi ambayo inajiandaa kwa uchaguzi.

Juhudi hizi zitasaidia kupunguza kuyumba kwa demokrasia, na kuwapa wananchi imani katika upigaji kura.Vile vile, hatua hizi zinafaa pia kuonekana katika mtandao wa jumbe fupi wa WhatsApp.Isiwe tu wakati wa uchaguzi ambapo udhibiti huu unashuhudiwa; jumbe zisizofaa huchapishwa wakati wote. Nairai Facebook kuzidisha jitihada zake ili kuwafungia nje wote wanaokiuka sheria za mitandaoni.

Isafishe mtandao wake kwa kutumia programu ya kiteknolojia inayoweza kutambua maneno ya chuki, matusi, vitisho vya mauaji, ukiukaji wa haki za binadamu, taasubi za kike na kiume, dhuluma za watoto na zile za kimapenzi na ubaguzi wa rangi.

Nazo kampuni zinazomiliki mitandao mingine ya kijamii – Twitter, YouTube, Vimeo, LinkedIn na TikTok – ziige mfano wa Facebook ili hatimaye mitandao ya kijamii iwe pahali pa amani kwa kila mtumizi.

  • Tags

You can share this post!

Masoko ya wazi yaruhusiwe katika kaunti zilizofungwa

Raila, Kalonzo wapeleka vita vyao Mt Kenya