• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:50 AM
Maskwota elfu tatu wafurushwa

Maskwota elfu tatu wafurushwa

BRIAN OCHARO na KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya watu 3,000 katika mtaa wa Kadzandani, Kaunti ya Mombasa wana hofu ya kufurushwa makwao baada ya kupoteza kesi kuhusu umiliki wa ardhi waliyozozania na mwekezaji wa kibinafsi.

Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Mombasa ilitupilia mbali ombi lao la kutaka kupewa umiliki wa ardhi hiyo ambayo walidai wameishi humo kwa zaidi ya miaka 12.Jaji Sila Munya alisema hawakutoa ushahidi wa kutosha kustahili kupewa ardhi hiyo wala hawakutoa maelezo mahsusi kuhusu wakati walipoingia kwenye shamba hilo.

Maskwota hao walidai kuwa waliingia katika ardhi hiyo kati ya mwaka wa 1930 na 1940 huku wengine wakidai kuwa walizaliwa miaka ya tisini na wazazi wao walioishi katika shamba hilo.“Sina ushahidi kabisa kuhusu madai yao ya umiliki wa ardhi hiyo. Madai ya umiliki wa ardhi hiyo hayana thibitisho,” jaji huyo alisema.

Korti imeamuru maskwota waondoke kwenye ardhi hiyo ndani ya siku 90 la si hivyo wamiliki wana ruhusa kuwafurusha. Ndani ya kipindi hicho, maskwota hao wamezuiliwa kufanya maendeleo yoyote wala uboreshaji wa majengo yaliyopo kwenye ardhi hiyo.

Baadhi ya familia zilizoathiriwa zilidai kwamba zilinunua baadhi ya vipande vya ardhi kwa Sh80,000 na zaidi mwaka wa 2008 na kujenga nyumba za kuishi na maduka.Bw Harshit Mulvantari Rawal aliyewasilisha kesi hiyo ili maskwota hao wafurushwe aliiambia korti kuwa marehemu Lalitchandra Pandya alinunua ardhi hiyo kwa Sh210,000 kutoka kwa Miguel Cassio na Hamilton Antao, ambao walikuwa wakimiliki shamba hilo.

Alisema walitumia shamba hilo kwa kilimo.Kwingineko, wamiliki wa ardhi ambako miradi mikuu ya kitaifa inanuiwa kuanza kujengwa au kukamilishwa katika Kaunti ya Lamu, wamedai serikali inatumia nguvu kutwaa ardhi hizo bila kuwafidia.

Wakizungumza wakati wa kikao cha kujadili mradi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Lokichar (Turkana) hadi Lamu, wakazi hao walilalamika kuwa maafisa wa polisi na wa jeshi la ulinzi (KDF) wamekuwa wakitumiwa na serikali kuwatisha na kuwahamisha wananchi kwa lazima kutoka kwa ardhi zao.

Wakazi hao waliohudhuria kikao katika eneo la Mokowe, wanalalamika kuwa serikali imekuwa ikipeleka matingatinga kwenye ardhi zao na “kusafisha” ardhi bila ya kuwahusisha wamiliki.Wengi wa walalamishi ni kutoka vijiji vya Mokowe, Hindi, Magogoni, Roka, Kibiboni, Bar’goni na maeneo mengine.

Wakiongozwa na msemaji wao, Bw Tonny Kimathi, walisema mara nyingi wameshindwa kujitetea kwani matingatinga yanayolima ardhi zao huwa yanalindwa na polisi na KDF.Hata hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alishikilia kuwa serikali imekuwa ikifuata njia zifaazo kisheria katika kutwaa ardhi za miradi Lamu.

Bw Macharia alisema mikutano imekuwa ikiandaliwa kukutanisha wananchi ili kujadiliana kuhusu miradi kabla ya ardhi zao kutwaliwa.“Tumekuwa tukiwashirikisha wananchi katika kila hatua zinazotakikana kabla ya ardhi za miradi kutwaliwa. Serikali haiwezi kumdhulumu mwananchi wake. Ikiwa wewe ni mmiliki halisi wa ardhi ambayo serikali inafaa kutwaa ili kufanikisha miradi lazima ufidiwe,” akasema Bw Macharia.

Mwenyeji mwingine, Bi Amina Khamis alisema ni vyema serikali kutekeleza usoroveya wa ardhi zote inazolenga na kuwafidia wenyeji kwanza kabla ya ardhi zao kutwaliwa kwa miradi husika.Bi Khamis alieleza masikitiko yake kwamba mara nyingi huwa wanakosa ushahidi wa umiliki wa ardhi zinazotwaliwa kwa miradi ya serikali Lamu kila wanapotafuta fidia zao kwa kuwa hawajapewa hatimiliki.

“Sisi hatuna hatimiliki za ardhi lakini huwa tuna miti tumepanda kwenye ardhi husika. Pia huwa na vibanda vyetu. Ikiwa serikali itavamia ardhi hizo na kuzisafisha kwa kutumia tingatinga, ushahidi huo tutaupata wapi? Ni vyema makadirio yafanywe na kisha kufidiwa kwanza kabla ya ardhi zetu kutwaliwa kufanikisha miradi,” akasema Bi Khamis.

Mzee Peter Mwaura ambaye ni Mwenyekiti wa Nyumba Kumi eneo la Hindi aliomba mikutano zaidi ifanywe baina ya wananchi, serikali na wawekezaji wa miradi ili kuwe na masikilizano kuhusu ardhi zinazonuia ili kuzuia uhasama.

“Tumejionea baadhi ya wamiliki wa ardhi za Bandari ya Lamu wakililia fidia zao hadi leo bila mafanikio. Hali hii inajenga chuki baina ya wananchi, serikali na wawekezaji. Ni vyema mikutano ya kila mara kuandaliwa ili mwananchi kujulishwa ni jinsi gani atapata haki baada ya ardhi yake kutwaliwa kufanikisha miradi,” akasema Bw Mwaura.

  • Tags

You can share this post!

Echesa alikuwa amemletea Ruto Wazungu wawili alipokamatwa,...

Masoko ya wazi yaruhusiwe katika kaunti zilizofungwa