• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Maswali tele yazuka kuhusiana na jinsi Kangogo alivyokufa

Maswali tele yazuka kuhusiana na jinsi Kangogo alivyokufa

Na LEONARD ONYANGO

KIFO cha mshukiwa wa mauaji Caroline Kangogo ambaye mwili wake ulipatikana Ijumaa bafuni, kimezua maswali tele.

Kangogo alikuwa afisa polisi wa cheo cha konstabo ambaye aliwahi kuhudumu katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi cha Mombasa, Kituo cha Polisi cha Kaloleni na Kituo cha Polisi cha Nakuru.

Mwili wa Kangongo ambaye amekuwa akisakwa na polisi kwa madai ya kuuwa wanaume wawili, wiki iliyopita, ulipatikana nyumbani kwao kijijini Anin, Tambach, Kaunti ya Elgeyo Marakwet saa mbili asubuhi.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Bw Patrick Lumumba, aliongoza kikosi cha maafisa wa polisi kufanyia uchunguzi eneo la tukio kabla ya kupeleka mwili katika mochari ya Hospitali ya Kaunti ya Iten.

Bw Lumumba alisema kuwa maafisa wa polisi wanachunguza jinsi Kangogo, ambaye amekuwa akiwindwa na maafisa wa polisi tangu Julai 5, mwaka huu, alirejea nyumbani kimyakimya na kisha kujifyatulia risasi bafuni bila familia yake kusikia.

Kulingana na Bw Lumumba, Kangogo hakuacha ujumbe wowote kabla ya kujitoa uhai.

“Bado ni kitendawili kwani hatujui namna Kangogo alirejea nyumbani kwao asubuhi na kujifyatulia risasi bila watu wa familia yake kumuona au kusikia,” akasema kamanda huyo wa polisi.

Maafisa wa polisi wanaamini kuwa Kangogo alijitoa uhai. Lakini baadhi ya wanaharakati wanashuku kuwa huenda aliuawa na watu wengine ambao waliacha mwili wake bafuni.

Kangogo anadaiwa kuua afisa mwenzake wa polisi John Ogweno jijini Nakuru kabla ya kufululiza hadi eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu, na kumuua Peter Ndwiga. Inaaminika kuwa Ogweno na Ndwiga walikuwa wapenzi wake.

Wazazi wake waliita maafisa wa polisi baada ya kupata mwili wa binti yao bafuni.

Kulingana na Kamishna wa Ukanda wa Bonde la Ufa, Bw George Natembeya, mwili wa Kangogo uligunduliwa na mama yake aliyekuwa akienda kuoga bafuni asubuhi.

Maiti ilikuwa imevalia nguo ambazo kamera ya CCTV ilimnasa akiwa amevalia alipodaiwa kuua Ndwiga katika lojing’i moja eneo la Juja mnamo Julai 5.

Je, inawezekana kwamba Kangogo hajawahi kubadilisha nguo kwa siku 12? Alitokea wapi Ijumaa asubuhi na kufululiza hadi nyumbani kwao na kisha kujitoa uhai?

Inawezekana alikuwa ametekwa nyara na watu fulani ambao baadaye walimpeleka kwao na kumuua? Mbona hakujisalimisha hata baada ya wakili John Khaminwa kujitolea kumwakilisha kortini kumtetea asikamatwe?

Inawezekana Ogweno na Ndwiga waliuawa na watu wengine ambao pia waliangamiza Kangogo ili wasifichue taarifa nyeti walizokuwa nazo?

Wataalamu pia wamehoji kwa nini hakukuwa na matone ya damu kwenye sehemu ya ukuta iliyokaribiana na shavu ambapo inaaminika kwamba risasi ilitokea?

Nani alifunika kichwa chake kwa kitambaa baada ya kufa? Mbona aliendelea kushikilia bastola hata baada ya kujifyatulia risasi?

Hayo ni baadhi ya maswali ambayo maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) watayatafutia majibu wakati wakiendesha uchunguzi wao.

You can share this post!

Dimba mlimani

Wabunge watishia kumtoroka Musalia