• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
Matumaini kiwanda kikipokea Sh30m

Matumaini kiwanda kikipokea Sh30m

Na VICTOR RABALLA

WAKULIMA wa miwa eneo la Nyanza, wamefurahishwa na hatua ya serikali kukipa kiwanda cha sukari cha Muhoroni Sh30 milioni ili kurekebisha mashine ya kusaga miwa.

Kiasi hicho ni asilimia 20 pekee ya kiwango cha fedha ambazo kiwanda hicho kiliomba serikali mnamo Machi 21, baada ya kuwekwa chini ya usimamizi wa mrasimu.

Kiwanda hicho kilikuwa kimeomba Sh150 milioni kuendelea na urekebishaji wa vifaa vyake.

Fedha hizo pia zinatarajiwa kuimarisha utendakazi wa kiwanda hicho ili kianze kurejelea shughuli zake, kabla usimamizi wake kutwaliwa na mwekezaji wa kibinafsi.

Meneja wa kiwanda hicho, Bw Francis Ooko, alisema kuwa wanalenga kurekebisha tanuri lake na pia kutoa zabuni kwa kampuni mbalimbali zenye nia ya kutekeleza ukarabati huo. Pia wanatarajia kununua tanuri jipya alisema.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Kilimo na Uzalishaji wa Vyakula (FAO), Bw Kello Harsama alitoa wito kwa usimamizi wa kiwanda hicho utumie Sh30 milioni ili kirejelee oparesheni zake kabla ya mwekezaji kutwaa usukani.

“Kwa kuwa kuna miwa na hitaji la kuongeza kiwango kinachosagwa kila siku, tunapendekeza kuwa shughuli kiwandani zirejelewe huku tukisubiri mwekezaji aanzishe kazi,” akasema Bw Harsama.

Kwa muda wa miaka mitano iliyopita, kiwanda cha Muhoroni kimekuwa kikikabiliwa na changamoto mbalimbali hasa matumizi ya mashine iliyozeeka kutokana na ukosefu wa fedha za kununua nyingine mpya.

Mara ya mwisho vifaa vya kiwanda hicho vilikarabatiwa na nyingine mpya kununuliwa ni kati ya 2016-2017, jambo ambalo limesababisha iwe vigumu kuendesha kazi yake.

Awali kiwanda hicho kilikuwa kikisaga tani 3,000 za miwa kila siku ila sasa kinasaga tani 1,000 pekee huku miwa mingi ikichelewa kusagwa.

“Bado tunaisukuma serikali ili ituongezee fedha zaidi ndipo ukarabati mwingine utekelezwe ili tusage miwa mingi,” akaongeza.

Kurekebishwa kwa mashine ya kiwanda cha Muhoroni kumefanyikawakati ambapo wakulima wanakodolewa macho na hasara tele kwa kukosa pa kupeleka miwa yao.

Viwanda jirani vya Kibos na Chemelil navyo pia vimekuwa vikikabiliwa na ukosefu wa hela na pia tanuri zao kuharibika jambo ambalo limepunguza kiasi cha miwa inayofikishwa kiwandani.

Kufikia mwisho wa wiki jana, ilikadiriwa kuwa wakulima walikuwa wamepoteza hadi Sh50 milioni baada ya kuachwa na zaidi ya tani 14,000 za miwa huku wakipanga foleni katika vituo vya kupima uzani eneo hilo.

You can share this post!

Wandani wa Ruto wamjibu Tuju

Waiguru ateuliwa kati ya wanawake 100 bora bara Afrika