• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
Mbinu mpya zinazotumiwa kudumisha usalama mitaani

Mbinu mpya zinazotumiwa kudumisha usalama mitaani

Na SAMMY KIMATU

MIKAKATI mizuri iliyowekwa na kubuni mbinu mpya kudhibiti usalama katika eneo la polisi la Makadara msimu wa sherehe kulizaa matunda huku visa vya uhalifu vikikosa kushuhudiwa.

Mkuu wa polisi eneo la Makadara, Bw Timon Odingo aliambia Taifa leo kwamba alishirikiana vizuri na mkuu wa Kitengo cha Upelelezi wa Jinai (DCIO), Bw Steven Muema Mutua.

Aidha, Bw Odingo aliongeza kwamba, kando na maafisa hao, walipangia askari wao kazi wakitumia magari ya kibinafsi ya usalama kama vile SG, G4S, Group 4, KK na kadhalika.

Bw Mutua aliongeza kwamba waliwapanga polisi waliovalia kiraia katika maeneo yaliyodaiwa kuwa sugu kwa usalama baada ya kupeleleza na kujua kila kona ambayo usalama ulidorora.

“Tuliweka askari wetu waliojihami kwa silaha na kuvalia kiraia kwenye maeneo sugu kwa uhalifu kabla, wakati na baada ya Krisimasi. Pia ongezeko la maafisa wetu wa kushika doria walikuwa chonjo saa 24/7 pamoja na raia kujitolea kutupasha habari kuhusu mipango ya wahalifu ambayo tulitibua kabla ya kutendeka,” Bw Mutua akanena.

Kwa kawaida, eneo la Makadara lina mitaa mingi ya mabanda ambayo hapo awali, kulishuhudiwa msururu wa ongezeko la visa vya uhalifu hasa mwezi Disemba kila mwaka.

Wananchi waliohojiwa walipongeza maafisa wa polisi wakisema ni ajabu mwaka huu kutoripotiwa visa vya uhalifu katika eneo la Makadara.

“Huu ni mwaka wa ajabu ambao hatukusikia watu wakiporwa pesa wakielekea sokoni, wakiwa steji wala kushuhudia nyumba kuvunjwa na wahalifu mitaani Disemba ya mwaka jana ikilinganishwa na miaka ya hapo nyuma,” Mwenyekiti wa usalama mtaa wa mabanda wa Mukuru-Hazina, Bw David Kiarie akasema.

Mwaka jana maafisa wa polisi waliewanasa washukiwa 15 katika maficho ya mtaani wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo wakidaiwa kujikusanya kupanga uhalifu.

Bw Odingo alithibitisha maafisa wake wakishirikiana na kitengo maalumu cha SPIV na wapelelezi wa jinai walifanya msako na kuwakamata washukiwa wote.

Isitoshe, mseto wa silaha mbalimbali ikiwemo risasi, visu, panga zilizolowa damu, kadi kadhaa za simu, rununu na stakabadhi za benki zilinaswa pia na polisi.

“Washukiwa hao 15 walipatikana na silaha walizotumia kuwahangaisha wakazi mitaani ya mabanda ya South B, mkabala wa barabara kuu kuelekea Mombasa, barabara ya Likoni, Entreprise, Lunga Lunga na Eneo la Viwandani,” Bw Odingo akanena.

Katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Lunga Lunga, washukiwa wengine 16 walinaswa wakihusishwa na kuwapora pesa wakazi kwa kuwatoza ada ya kutumia stima.

Vilevile, duru za polisi zilieleza kwamba washukiwa walitumia nguvu kuitisha wahudumu wa pikipiki pesa sawia na wahudumu wa matatu katika steji mkabala wa barabara ya Lunga Lunga.

  • Tags

You can share this post!

Wanyakuzi wa shamba la Rais washtakiwa

Mwanamke aponea kifo risasi ya polisi ilipomkosa

T L