• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Mbinu wanazotumia walaghai kuingiza bidhaa kutoka Somalia

Mbinu wanazotumia walaghai kuingiza bidhaa kutoka Somalia

Na BRIAN OCHARO

WAFANYABIASHARA walaghai wamegundua mbinu mpya ya kuingiza bidhaa humu nchini kutoka Somalia kupitia Bahari Hindi.

Mamlaka ya Ushuru Nchini (KRA) inasema bidhaa hizo hupakiwa katika boti ndogo zenye injini kabla ya kusafirishwa hadi Bandari ya Mombasa bila kulipiwa ushuru.

Baadaye bidhaa hizo hupenyezwa katika masoko ya Kenya na hivyo kuuzwa kwa bei nafuu.

Sakata hii imefichuliwa baada ya wanajeshi wa kikosi cha wanamaji kunasa chombo kimoja kilichojaa bidhaa baharini mnamo Mei 2021.

Stakabadhi ambazo tuliweza kuona zinaonyesha kuwa Mv Tima Fena ilinaswa mnamo Mei 17, na maafisa wa jeshi la wanamaji likipakua bidhaa kutoka jimbo la Jubaland, nchini Somalia.

Kwa kutumia vifaa maalum, wanajeshi waliweza kuwaona wahudumu wa chombo hicho kwa umbali wakipakuwa bidhaa na kuziweka katika boti ndogo kisha kuzisafirisha hadi bandarini.

“Baada ya meli hiyo kukaguliwa, iligunduliwa kuwa ilikuwa imebeba mitungi 77 ya mafuta ya kupikia (ya lita 20) na tani 17 za vyuma vikuukuu kutoka Somalia; bidhaa zote za thamani ya Sh908,064,” KRA ikasema.

Msimamizi wa meli hiyo, Bw Yusuf Mohamed Abdallah, alikamatwa na maafisa wa jeshi la wanamaji.

Mnamo Ijumaa, alifikishwa katika mahakama moja ya Mombasa na kufunguliwa mashtaka ya kuingiza bidhaa nchini kinyume cha kipengele cha 199 (b) cha Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Forodha, 2004.

Kulingana na stakabadhi ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani, Bw Abdalla alishtakiwa kwa kuingiza nchini bidhaa kutoka jimbo la Jubaland, Somalia kinyume cha sheria.

Alitenda kosa hilo mnamo Mei 17, 2021.Hata hivyo, alikana mashtaka hayo aliyosomewa na Hakimu Mkuu wa Rita Amwayi.Aliachiliwa huru kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.

Endapo atapatikana na hatia, Bw Abdallah ataadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh700,000. Vile vile, huenda meli hiyo na bidhaa hizo zikatwaliwa na serikali.

Kulingana na KRA, wahudumu wa meli hiyo walijaribu kupakuwa bidhaa hizo baharini kabla ya kufika Mombasa.

Hii ni kutokana na marufuku iliyoko sasa dhidi ya kuingizwa kwa bidhaa zozote kupitia mpaka wa Somalia na Kenya.

Mnamo 2019, Kenya ilifunga mpaka wake na Somalia na hivyo kupiga marufuku biashara katika eneo la mpaka wake na nchi hiyo jirani. Vile vile, serikali ya Kenya ilifunga mipaka yake na Somalia katika kaunti za Lamu, Mandera, Wajir na Garissa.

Kufungwa kwa maeneo hayo ya mipaka ilikuwa ni sehemu ya mikakati ya kiusalama kuzuia mashambulio kutoka kwa wanamgambo wa al-Shabaab.

Iliripotiwa kuwa magaidi hao walivuka mpaka na kuingia nchini Kenya kabla ya kutekeleza mashambulio yaliyochangia vifo na majeruhi ya watu kadha.

Aidha, ilidaiwa kuwa vijana kutoka Kenya walitumia mipaka hiyo kuingia Somalia kujiunga na mafunzo ya ugaidi.

You can share this post!

TAHARIRI: Ripoti ya Kemsa inakatisha tamaa

TAHARIRI: Sakata ya Kemsa inakatisha tamaa