• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Mbunge ataka wajane waoane ili kupunguza upweke

Mbunge ataka wajane waoane ili kupunguza upweke

NA TITUS OMINDE

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti ya Trans Nzoia Lilian Siyoi amewataka wajane kuoana ili kupunguza idadIi ya wajane inayoongezeka katika kaunti hiyo.

“Ninawahimiza wajane kuoana na wajane wenzao tena, hasa wale walio na umri wa chini ya miaka 60. Si vyema kwa watu walio chini ya umri wa miaka 60 kujiita wajane ilhali wanaweza kuolewa tena na kufurahia matunda ya ndoa,” alisema Bi Siyoi.

Hata hivyo, Bi Siyoi alikashifu ongezeko la walaghai wanaojifanya wajane kwa lengo la kunufaika na miradi ya serikali inayolenga wajane.

Akizungumza Jumapili katika kaunti ndogo ya Cherangan, kiongozi huyo alisema idadi ya wajane ghushi inaongezeka nchini na hivyo kuwa vigumu kwa serikali kusaidia wajane halisi.

“Rasilimali chache zilizopo kusaidia wajane zinatumika vibaya kutokana na watu wanaojifanya wajane kwa kughushi vyeti vya vifo ili kuwalaghai maafisa wa serikali waandikishwe katika mradi wa serikali unaolenga wajane,” alisema Bi Siyoi.

Bi Sioyi aliitaka idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI ) kuchunguza asili ya vyeti feki vya vifo vinavyotumiwa kuwanyima wajane halisi fursa ya kufaidika na miradi ya serikali inayolenga wajane.

  • Tags

You can share this post!

Diwani wa UDA ashtakiwa kumteka nyara na kumpiga mwalimu

KRA yaondolea Kidero kesi ya ushuru wa Sh427 milioni

T L