• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
KRA yaondolea Kidero kesi ya ushuru wa Sh427 milioni

KRA yaondolea Kidero kesi ya ushuru wa Sh427 milioni

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa zamani wa Nairobi sasa anaweza kupumua baada ya Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) kumuondolea kesi ya ushuru wa mamilioni ya pesa iliyokuwa ikimkabili.

Akiondolewa lawama, Mahakama ya Rufaa ilikubali cheti cha maafikiano kati ya Dkt Kidero na KRA kilichoonyesha jinsi gavana huyo alivyolipa deni hilo la kodi.

Mawakili James Oduol anayemwakilisha Dkt Kidero na Leparashao Naeku Patricia waliikabidhi mahakama cheti cha makubaliano.

Katika cheti hicho Dkt Kidero na Kamishna wa ushuru katika KRA walikubaliana badala ya Dkt Kidero kulipa Sh427,269, 795 atalipa Sh19,489,183 ikiwa ni pamoja na deni halisi la Sh12,038.982.

Pia Dkt Kidero atalipa riba ya Sh5,036,405 na faini ya Sh2,407,796.

Deni hili la kodi ni la miaka 2011, 2012 na 2015. Dkt Kidero alikuwa amekabwa koo na KRA kulipa deni hili kisha mawakili Oduol na Leparashao wakaomba mahakama ya rufaa iwape fursa mshtakiwa na mlalamishi wasikizane.

Mkataba huo uliwasilishwa katika mahakama ya rufaa mnamo Agosti 4,2023.

Kufuatia kutiwa sahihi kwa mkataba huo mbele ya mahakama, deni hilo lilitiwa muhuri kwamba limelipwa.

Mzozo wa KRA na Dkt Kidero ulianza 2016 baada ya mkaguzi wa hesabu kusema anatakiwa alipe serikali kodi ya Sh680milioni.

Dkt Kidero aliwasilisha rufaa kupinga agizo hilo Katika rufaa yake alidai Sh423milioni zilikuwa pesa alizopewa na marafiki za kugharamia kampeini yake ya 2013.

Baada ya kamati ya rufaa kukubaliana na Kidero, KRA iliwasilisha rufaa nyingine katika mahakama kuu.

KRA ilimshinda Dkt Kidero huku mahakama kuu ikisema gavana huyo wa zamani hakuthibitisha pesa hizo Sh423milioni zilikuwa michango ya kampeini.

KRA ilikubaliwa kudai kodi ya Sh427.4milioni.

Mbali na kesi hii ya kodi Dkt Kidero anakabiliwa na kesi za ufisadi wa Sh350milioni na nyingine ya ubadhirifu wa Sh58 milioni wakiwa na washukiwa sita waliokuwa wahasibu katika serikali yake Dkt Kidero aliyekuwa miongoni mwa manaibu mawaziri 50 walioteuliwa na Rais William Ruto kabla ya kufutwa kazi na mahakama kuu alishtakiwa upya mbele ya Hakimu Mkuu Bw Felix Kombo katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi.

Dkt Kidero, Bw Kariuki, wahasibu sita na wakurugenzi wawili wa kampuni ya The Cups Limited John Ngari Wainaina na George Wainaina Njogu walikanusha mashtaka 15, Dkt Kidero alikabiliwa na mashtaka ya kujipatia Sh14.4milioni pesa za umma.

Hakimu alifahamishwa pesa hizi zilikuwa sehemu ya Sh58milioni zilizokuwa zimelipwa kampuni ya marehemu wakili Steven Kariuki Mburu 2014.

Dkt Kidero pia alishtakiwa kujitajirisha na pesa alizojua zimepatikana kwa njia ya ufisadi.
Bw Kariuki aliyekuwa Meya wa Jiji la Nairobi alikabiliwa na shtaka la kutia kibidoni Sh8.9 milioni kutokana na kitita hicho cha Sh58milioni kilichokuwa kimeporwa kaunti ya Nairobi Januari 2014.

Hakimu alifahamiwa Sh17milioni zilitumika kununua ardhi na Sh2milioni kutumika kulipia deni la aliyekuwa diwani Mutunga Mutungi.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge ataka wajane waoane ili kupunguza upweke

Kampuni iliyomshtaki Amadi kuhusu sakata ya dhahabu yahofia...

T L