• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 9:39 PM
Mbunge ataka wakongwe walindwe kwa njia bora

Mbunge ataka wakongwe walindwe kwa njia bora

NA LAWRENCE ONGARO

MBUNGE wa Thika Alice Ng’ang’a ametoa wito wakongwe waongezwe fedha za Inua Jamii ili kuinua maisha yao.

Mbunge huyo anapendekeza fedha hizo ziongezwe kutoka Sh2,100 hadi 3,500 ili waweze kujikimu kimaisha.

Bi Ng’ang’a ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya kulinda fedha za wakongwe alisema kwa sababu hali ya maisha imepanda maradufu, ni vyema maslahi ya wakongwe hao yalindwe vilivyo.

“Tunaelewa vizuri ya kwamba hali ya maisha imepanda maradufu na kwa hivyo ni vyema kuongeza kiwango cha fedha wanazopokea wakongwe hao,” alifafanua mbunge huyo.

Aliyasema hayo mnamo Jumatano alipogawa chakula kwa wakongwe katika maeneo ya Starehe na Ofafa mjini Thika.

Mbunge wa Thika Alice Ng’ang’a ametoa wito wakongwe waongezwe fedha za Inua Jamii ili kuinua maisha yao. PICHA | LAWRENCE ONGARO

 

Wakongwe hao walipokea unga wa ugali, mchele, maziwa na biskuti ili wale wakati huu ambapo makali ya njaa yanahangaisha wengi nchini.

Kwa kawaida wakongwe waliofikisha umri wa miaka 70 ndio wanaonufaika.

Hata hivyo alisema kwa muda mrefu wakongwe wengi wamekuwa wakipokea fedha hizo lakini kulingana na orodha iliyoko, majina ya wakongwe wapatao 250,000 hayako kwenye orodha hiyo tangu mwaka wa 2017.

Alisema wakongwe wapatao 8,192 wameorodheshwa katika malipo hayo huku majina hayo yakiwa hayaambatani ipasavyo.

Kulingana na mbunge huyo, wakongwe wapatao 93,565 ambao wakistahili kunufaika wamekuwa hawapati fedha hizo inavyostahili.

Mbunge huyo alisema wakongwe wengi wameathirika na njaa hasa ikitiliwa maanani kuwa janga la Covid -19 liliyumbisha uwezo wa Wakenya wengi.

Alitoa wito kwa kampuni zilizoko katika eneo la Thika kujitokeza ili kusaidia wasiojiweza hasa wakongwe.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Ruto hajatimiza ahadi kuhusu bima ya NHIF

Serikali yafungua kituo kudhibiti uvamizi wa nzige

T L