• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mbunge na abiria 30 wanusurika ndege ikiharibika angani

Mbunge na abiria 30 wanusurika ndege ikiharibika angani

Na KALUME KAZUNGU

TAHARUKI ilitanda miongoni mwa abiria waliokuwa ndani ya ndege ya kampuni ya Skyward kutoka Lamu kuelekea Nairobi, iliposemekana kupata hitilafu muda mfupi baada ya kupaa angani.

Miongoni mwa abiria zaidi ya 30 waliokuwa kwenye ndege hiyo ni Mbunge wa Matuga, Bw Kassim Sawa Tandaza.

Kisa hicho kilitokea mwendo wa saa kumi na robo jioni, Jumatatu.

Ililazimu rubani wa ndege kujitahidi kurejea kwenye uwanja wa Manda, ambapo abiria walipandishwa ndege nyingine ili kuendelea na safari yao.

Hata hivyo baadhi ya abiria, akiwemo Bw Tandaza waliamua kukatiza safari yao baada ya mkosi huo kutokea.

Ilidaiwa hitilafu ilitokea katika moja ya injini za ndege hiyo.

Juhudi za kupata mawasiliano kutoka kwa kampuni ya Skyward ziligonga mwamba kwani maafisa husika walioko Lamu walidinda kuzungumzia tukio hilo.

Katika mahojianio na Taifa Leo, Bw Tandaza alisema walisikia mlipuko usio wa kawaida dakika chache baada ya kupaa angani.

Baadaye rubani aliwajulisha abiria kuwa watulivu kwani ndege ilikuwa na kasoro ya mojawapo ya injini yake na kwamba italazimika warudi tena uwanja wa Manda na kuchukua ndege nyingine.

“Ilikuwa hali ya kutisha. Baada ya mlipuko na tangazo, sote tulikuwa na wasiwasi. Ni mara yangu ya kwanza kukumbana na hitilafu ndani ya ndege ikiwa angani. Wa kuomba aliomba, wa kushika Biblia au Qurani alifanya hivyo. Hata wa kulia pia walilia. Tunashukuru kwamba ndege mwishowe ilitua na sote tukatoka salama,” akasema Bw Tandaza.

Mbunge huyo aidha aliiomba Mamlaka ya Kusimamia Ndege nchini (KCAA) na wengineo wanahusika na usalama wa angani nchini kuwa makini enzi hizi ambapo idadi ya mashirika ya ndege yaongezeka.

Abiria mwingine, Bw Mohamed Omar alimshukuru Maulana kwa kuwakinga dhidi ya kifo ambacho kilikuwa kimewakodolea macho.

“Kile nimeshuhudia leo mimi hukiona tu kwa sinema. Sikuwahi kufikiria kwamba kingetokea maishani mwangu. Wametubadilishia ndege lakini siendi ng’o. Nimekatiza hii safari. Leo ilikuwa siku ya mikosi,” akasema Bw Omar.

Si mara ya kwanza abiria kukumbwa na mshtuko wakati wakiwa kwenye harakati za kusafiri kwa ndege kwenye uwanja wa Manda, Lamu.

Mnamo Agosti,2019, abiria 36 waliokuwa wameabiri ndege ya kampuni ya Fly540 walishtuka pale ndege hiyo iliposhindwa kupaa angani wakati ikijaribu kuondoa baada ya mojawapo ya magurudumu yake kugwama kwenye shimo.

Ililazimu abiria kushuka kwanza na wahudumu wa uwanja huo wa ndege kuisukuma ndege hiyona kulitoa gurudumu shimoni kabla ya safari kuendelea baada ya kucheleweshwa kwa zaidi ya dakika 20.

  • Tags

You can share this post!

Athari za kutumia vyombo na bidhaa za plastiki

Wafuasi wa Ruto wamtongoza Kingi ajiunge na...