• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Athari za kutumia vyombo na bidhaa za plastiki

Athari za kutumia vyombo na bidhaa za plastiki

Na MARGARET MAINA

[email protected]

PLASTIKI ina nafasi kubwa kwenye jamii ya sasa.

Hutumika kwenye magari, vyombo vya nyumbani, vifaa vya watoto kuchezea, simu, na kadhalika. Kwa hivyo sio rahisi mtu kumaliza siku nzima bila kutumia kifaa chochote cha plastiki.

Usitumie kabisa vyombo vya plastiki kuchemshia au kuwekea vyakula vya moto kama chai, maziwa, supu, maji, na ugali. Hii ni kwa sababu plastiki inapopata moto, huzalisha kemikali iitwayo BPA (Bisphenol A) ambayo ikiingia mwilini husababisha magonjwa mengi kwa binadamu; miongoni mwake ni:

  • magonjwa ya ini
  • magonjwa hatari ya moyo
  • kisukari
  • magonjwa ya kizazi kwa jinsia zote
  • kuathirika kwa nguvu za kiume
  • pumu huongezeka kwa wagonjwa wa pumu
  • huathiri mfumo wa fahamu na kusababisha kupoteza kumbukumbu.

Zamani mababu zetu walikula vitu vya asili na kutumia vitu vya asili na ndiyo maana hawakuwa wanasumbuliwa na magonjwa mengi.

Mababu zetu waliishi hadi umri wa miaka mingi kwani hawakuwa na vyakula vya viwandani, yaani vyakula vyenye kubuniwa na kutengenezwa na binadamu, ambavyo vingi ni vyakula vyenye kemikali za sumu.

Vyakula hivyo vinaweza kuliwa lakini ni muhimu kuzingatia unywaji wa maji mengi ambapo kiwango cha chini ni lita moja kwa siku. Pia ni muhimu kula matunda mengi na mboga za majani.

Hakikisha huweki vyakula vya moto kwenye vyombo vya plastiki nyumbani kwako.

Ni ukweli kuwa plastiki zina matumizi makubwa lakini pia zina athari kwenye afya yetu na mazingira. Ni vyema ukatumia vyombo vya udongo, kioo kwa maana ya glasi, mbao au hata alumini (aluminium) badala ya plastiki.

Madhara ya plastiki huonekana baada ya muda mrefu ambapo unaweza kuvitumia vyombo hivyo na kutoona madhara yake katika muda mfupi lakini baadaye, utapata ugonjwa ambao utashindwa kujua chanzo chake.

You can share this post!

AFYA: Umuhimu wa mazoezi kwa wajawazito

Mbunge na abiria 30 wanusurika ndege ikiharibika angani