• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:07 PM
Mbunge Richard Onyonka ajisalimisha kwa DCI mjini Kisii

Mbunge Richard Onyonka ajisalimisha kwa DCI mjini Kisii

NA WYCLIFFE NYABERI

MBUNGE wa Kitutu Chache Kusini Richard Onyonka, Jumanne asubuhi alijisalimisha kwa maafisa wa upelelezi mjini Kisiii kutokana na matamshi aliyoyatoa kwenye mkutano mmoja wa kisiasa wikendi iliyopita.

Mkurugenzi mkuu wa mashataka ya umma (DPP) Noordin Haji, aliagiza idara ya polisi kumchunguza mbunge huyo kufuatia matamshi aliyoyatoa na yanayodaiwa kuwa ni uchochezi.

Katika mkutano wa eneobunge la Nyaribari Chache, kaunti ya Kisii, Bw Onyonka alikashifu kauli ya ‘madoadoa’ iliyotolewa na Seneta wa Meru Mithika Linturi. Pia alimkemea Naibu Rais William Ruto.

“Ningependa kumwambia ndugu yangu William Ruto, usijaribu kuharibu Kenya kama nchi kwa sababu unataka uongozi kwa kifua. Mkisii anajitafutia. Mkisii amejipanga Kenya nzima. Ukigusa Mkisii tutakutafuta hata wewe mahali utakuwa… Wakati huu ukigusa Mkisii hata mmoja hutaweza kuja hapa Kisii,” Bw Onyonka akasema.

Video yenye maneno hayo ilianza kusambazwa mitandaoni na baada ya DPP kuiona, alitaka mbunge huyo achunguzwe na faili yake kupeanwa kwa afisi yake ndani ya kipindi cha siku saba.

“Marejeleo yanafanywa kufuatia video inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii ambapo Bw Onyonka anahutubia umati katika kaunti ya Kisii. Kauli kwenye video hiyo zinaweza kuwa zinakiuka Katiba ya Kenya ya mwaka 2010,” ikasema sehemu ya barua ya Bw Haji.

Alipojiwasilisha katika kituo cha polisi, aliandamana na mbunge wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati, pamoja na mawakili wake wakiongozwa na Mabw Wilkins Ochoki na Ratemo Ombui.

Aliandikisha taarifa fupi kwa maafisa wa upelelezi na kuachiliwa.

Mawakili hao walisema mkuu wa idara ya upelelezi eneo la Kisii Bi Beatrice Kabaila aliwaashiria kwamba huenda Bw Onyonka akatakiwa kufika katika makao makuu ya DCI jijini Nairobi kutoa taarifa zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Kenya Power yatoa hakikisho tatizo la umeme kukatika...

SHINA LA UHAI: Hofu ya ongezeko la matatizo ya kusikia...

T L