• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Mbunge wa zamani apongeza vijana kwa kuweka akiba hadi kujenga nyumba za kukodisha

Mbunge wa zamani apongeza vijana kwa kuweka akiba hadi kujenga nyumba za kukodisha

NA LAWRENCE ONGARO

VIJANA wa kiume na wa kike kwenye kikundi cha watu 15 wamejizatiti na kuweka fedha za akiba hadi wakajenga nyumba za kukodisha.

Vijana hao walijikusanya kwa kikundi cha RIBAZI HOMES Sacco kuweka fedha zao hadi kufikia Sh4 milioni.

Mwenyekiti wa kikundi hicho Bw George Maina alisema iliwabidi wavumilie na kujinyima kabisa kabla ya kukusanya kiasi hicho cha fedha.

“Baada ya kuweka kwenye hazina yetu kiasi cha Sh4 milioni ilitubidi tuchukue mkopo wa Sh 2 milioni kutoka kwa kampuni ya J-Hela ili tuweze kuendesha mradi wetu wa kujenga nyumba za kukidisha eneo la Gachie lililoko Kiambaa kaunti ya Kiambu,” alifafanua Bw Maina.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya J- Hela Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema hatua waliyochukua na  vijana hao ni msingi dhabiti wa kimaisha kwa sababu kikundi hicho kitaendelea kupata mapato yao kupitia kodi ya nyumba.

“Ninawahimiza vijana popote walipo waungane kwa vikundi na kutafuta mikopo kupitia J-Hela. Niko tayari kuinua mipango ya vijana ambao wako katika vikundi na wangetaka  kujiendeleza,” alisema Bw Wainaina.

Mwenyekiti wa vijana hao Bw Maina alisema nyumba hizo zimejengwa katika eneo la ekari moja huku wakiwa na matumaini makubwa kuwa wapangaji watajitokeza  ili kuanza kuishi huko.

“Sisi kama vijana tuliungana na sasa tumeanza kuona matunda ya mipango yetu. Kwa hivyo tunawahimiza  vijana wengine popote walipo wafanye hima kuungana na kuanza miradi tofauti zitakazowasaidia kimaisha,” alieleza mwenyekiti huyo.

Alisema safari yao ya kuungana pamoja haikuwa rahisi sana kwani ilikuwa na panda shuka tele.

“Hata hivyo baada ya kuvumilia masaibu tulioyapitia tuna imani ya kuwa tutakula matunda ya jasho letu,” alifafanua Bw Maina.

Naye Bw Wainaina alisema J-Hela imenufaisha watu wengi kuinua biashara zao na pia kutekeleza mahitaji mengine muhimu.

Aliwahimiza vijana popote walipo wasitegemee kuajiriwa bali waungane na wafikirie jambo muhimu la kufanya ili wafanikishe hali yao ya baadaye maishani.
  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Juhudi zaidi zahitajika kukabili kansa ya...

Raila atangaza makabiliano

T L