• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
MCAs wapandisha joto la kudai nyongeza ya malipo

MCAs wapandisha joto la kudai nyongeza ya malipo

NA DERICK LUVEGA

MADIWANI wameongeza shinikizo za kutaka kuongezwa mishahara yao kutoka Sh144, 376 hadi Sh400,000 kwa mwezi.

Juhudi hizo zinaendeshwa na Baraza la Maspika wa Kaunti (CAF) wakati ambapo nchi inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.

Madiwani katika Kaunti ya Vihiga wakiongozwa na Spika Chris Omulele wameongeza sauti yao kwenye shinikizo hizo.

Madiwani hao 36 wamejiunga na wenzao nchini kote wakitaka kuongezwa mishahara yao na bajeti ya hazina ya kustawisha wadi.

Bw Omulele, ambaye ni mwanchama wa CAF, alisema kuwa madiwani wanataka kukutana na Rais William Ruto ili kuendeleza mpango huo.

Shinikizo hizo zilianzishwa na CAF Novemba mwaka uliopita. Hapo jana, Bw Omulele alisema kuwa madiwani wanataka kufanya kikao na Rais ili “kumweleza masuala muhimu yanayowahusu”.

“Madiwani wanalipwa mishahara midogo sana. Wanapaswa kuwa na kikao na viongozi wa kitaifa ili hali hii kuimarishwa,” akasema Bw Omulele.

“Mshahara wa sasa hauwezi kuwatosheleza madiwani kwani kinyume na wabunge, daima huwa wanatangamana na watu wao katika wadi. Malipo ya madiwani hao ni duni na wanateseka sana. Siogopi kusema hili kwani huwa ninajadiliana nao kila siku. Ni mjadala ambao lazima tuwe nao,” akaongeza Bw Omulele, aliyeandamana na madiwani wote kutoka kaunti hiyo.

Bw Omulele alisema alikuwa akizungumza kwa niaba ya madiwani wote wanaohisi kwamba itakuwa vizuri wafanye kikao na Rais ili kusuluhisha matatizo yao haraka.

Juhudi za madiwani zaidi ya 2,000 kote nchini kushinikiza kuongezwa mishahara zitaathiri mwelekeo na hali ya nchi, ikizingatiwa kuwa serikali inatumia fedha nyingi kulipia madeni.

Mwishoni mwa mwaka 2022, Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Dkt Patrick Njoroge aliwaambia wabunge kuwa kwa kila shilingi moja inayokusanywa kama ushuru, senti 40 huwa zinatumika kulipia deni la kitaifa.

Ikiwa madiwani wataongezewa mishahara kama wanavyoshinikiza, basi mlipaushuru atatumia Sh32 bilioni zaidi kutimiza mahitaji yao kwa miaka mitano ijayo.

Hapo awali, madiwani wamekuwa wakilalamika kuwa kuna tofauti kubwa ya kimalipo baina yao na wabunge ilhali huwa wanatekeleza majukumu sawa, kama vile kuangalia utendakazi wa serikali, uwakilishi na kutengeneza bajeti.

Kando na mshahara wao wa Sh144, 366 madiwani huwa na bima ya afya ya Sh3 milioni ikiwa atalazwa hospitalini, bima ya Sh200,000 ya maradhi ya kawaida, Sh100,000 kwa madiwani wanaojifungua na Sh50,000 za matibabu ya meno na macho.

Bw Omulele pia alisema madiwani wanataka hazina ya kustawisha wadi kuwekwa kwenye sheria ili kuwasaidia kuanzisha miradi.

  • Tags

You can share this post!

Mzozo kuhusu mpaka watesa watoto shuleni

Wito kwa wenye uwezo wamsaidie mvulana aliyezoa 306 aingie...

T L