• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Middlesbrough yadengua Tottenham FA

Middlesbrough yadengua Tottenham FA

Na MASHIRIKA

CHINI YA kocha Chris Wilder, Middlebrough waliendeleza makali yao dhidi ya miamba wa soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kudengua Tottenham Hotspur kwenye raundi ya tano ya kipute hicho kwa bao 1-0 ugani Riverside na kuingia robo-fainali kwa mara ya kwanza tangu 2017.

Mshindi wa kipute hicho alipatikana katika dakika ya 107 baada ya pande zote mbili kuingia muda wa ziada zilipotoshana nguvu kwa sare tasa kufikia mwisho wa dakika 90. Middlesbrough walishuka dimbani wakiwa na motisha tele ikizingatiwa kwamba walibandua Manchester United kwenye raundi ya nne.

Bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo lilifumwa wavuni na Josh Coburn baada ya kushirikiana vilivyo na Matt Crooks ambaye pia alimshughulisha vilivyo kipa Hugo Lloris.

Yalikuwa matarajio ya Spurs kwamba kocha Antonio Conte angewaongoza kutia kapuni Kombe la FA msimu huu na hivyo kutamatisha ukame wa kipindi cha miaka 14 bila taji lolote.

Middlebrough wanaoshiriki Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza (Championship) sasa wamshinda mechi nane mfululizo ugani Riverside.

Middlebrough walidengua Man-United katika raundi ya nne ya Kombe la FA kwa penalti 8-7 baada ya kuambulia sare ya 1-1 mwishoni mwa muda wa ziada. Conte alijilaumu mwishoni mwa mechi dhidi ya Middlesbrough kwa kuwajibisha kikosi sawa na alichokitegemea katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Leeds United kwenye EPL mnamo Februari 26, 2022.

Spurs hawajawahi kunyanyua taji la kipute chochote tangu watawazwe wafalme wa League Cup mnamo 2008. Kikosi hicho sasa kimepoteza mechi saba kati ya 13 zilizopita mwaka huu wa 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Hatua ya Raila kusaliti washirika yahujumu juhudi zake za...

Man-City watinga robo fainali za FA

T L