• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Mke amhadaa mumewe kuwa alitekwa

Mke amhadaa mumewe kuwa alitekwa

Na CECIL ODONGO

MAKACHERO kutoka Idara ya Upelekezi Nchini (DCI) Jumatano walimkamata mke ambaye alihepa ili kuponda raha na mwanaume mdogo kwake kiumri kisha akamhadaa mumewe kuwa alikuwa ametekwa nyara.

Polisi walimnyaka Bi Jane Wairimu Ndung’u ambaye alitoweka Ijumaa iliyopita na kumwaacha mumewe Brian Mutuku akiwa amejawa na wasiwasi mwingi kuhusu alikokuwa.

Siku hiyo, Bw Mutuku alipokea simu kutoka kwa mkewe ambaye alidai alikuwa mikononi mwa watekaji nyara waliokuwa wakidai kitita cha Sh200,000 ili kumwaachilia huru. Baada ya kupokea habari hizo za kustusha, Bw Mutuku alielekea katika kituo cha polisi cha Embakasi ambako alipiga ripoti kuhusu kutekwa nyara kwa mke wake mpendwa.

“Alidai kuwa alikuwa amekamatwa alipokuwa akitembea kwenye barabara ya Loita katikati mwa jiji la Nairobi,” ikasema taarifa ya DCI.

Hata hivyo, makachero walipokuwa wakiwaandama washukiwa wa utekaji nyara, Bw Mutuku na jamaa zake walichangisha Sh17,000 kisha kuwatumia wakora hao.

Huku makachero wakiendelea na kazi yao, familia haikuwa imefahamishwa kuwa Bi Wairimu alikuwa akila raha na mwendeshaji teksi ambaye alitambuliwa kwa jina Richard Mogire. Wawili hao walikuwa wakiishi pamoja katika chumba kimoja eneo la Malaa, Kaunti ya Machakos.

Familia nayo iliendelea na mchango wao na kutuma Sh40,000 tena mnamo Jumatatu, ikiwa na matumaini kuwa Bi Wairimu angeachiliwa huru.

Wawili hao walisafiri hadi Mtito Andei ili kutoa pesa hizo, hiyo ikiwa sehemu ya mikakati yao ya kufanya kazi ya makachero iwe vigumu zaidi kuwapata.

Makachero walipokuwa wakipanga kuwatia mbaroni, Bw Mutuku alipokea simu kutoka kwa mpenziwe ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jomo Kenyatta ambaye alimkumbusha kuhusu ahadi yake kwamba alifaa ampeleke aburudike wikendi hiyo.

Licha ya kusitasita na kumweleza kuwa alikuwa na dharura, mwanachuo huyo alisisitiza kuwa lazima mpango wa awali uendelee la sivyo, akatize uhusiano na Bw Mutuku.

Ili kuepuka kukamatwa kwake, mwanamume huyo alitumia gari jingine kando na lile alilokuwa ametumia kusafirisha Bi Wairimu kumchukua mwanafunzi huyo.

“Alibadilisha gari kisha akamchukua mpenzi chuoni na kuenda naye chumba ambacho alikuwa akikaa na Wairimu,” ikaongeza taarifa hiyo.

Watatu hao walinyakwa mjini Sagana Jumatano na wanaendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Embakasi wakisubiri kufikishwa kortini.

Bi Wairimu alifafanua kuwa alimhadaa mumewe ili kuepuka watu waliokuwa wakimdai alipe madeni aliyoyachukua na kutumia tukio hilo kupata pesa alizokuwa akidaiwa.

You can share this post!

Kikosi cha Uganda chawasili kwa mechi ya kufuzu kushiriki...

Bei ya juu ya gesi yasukuma Wakenya kukumbatia makaa, kuni