• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Mkulima anavyokabili kero ya mazao mbichi ya shambani kuharibika kwa kuyaongeza thamani

Mkulima anavyokabili kero ya mazao mbichi ya shambani kuharibika kwa kuyaongeza thamani

Na SAMMY WAWERU

JEFF Mundia ambaye ni Meneja wa Nairobi Farmers Market, soko lililoko Kiambu Road, kiungani mwa jiji la Nairobi pia ndiye msimamizi wa duka la familia yake.

Aidha, familia yake ni wakulima Kaunti ya Tharaka Nithi. Kwenye ekari kumi, hukuza matunda kama vile; mapapai, karakara, ndizi, maparachichi na pia matikitimaji.

Vilevile, huzalisha mazao mengine kama maboga, vitunguu, nyanya na miwa.Huku mengi ya mazao yakiwa yanayoharibika haraka baada ya mavuno, kulingana na Jeff duka hilo limewasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia wateja.

“Kando na bidhaa tunazolima, pia hununua mazao ya wakulima wengine,” asema.Hatua ya kuwa na duka kiungani mwa jiji la Nairobi imewasaidia kukwepa kero ya mawakala, ambao wamevamia soko la bidhaa za kilimo.

Licha ya mpango huo unaoonekana kuzaa matunda, bidhaa wanazouza hazina uhakika wa asilimia mia kwa mia kununuliwa zikaisha. Baadhi huharibika.Jeff anasema ili kuepuka hasara, The Farm Outlet huongeza mazao thamani kwa kutengeneza sharubati.

Baadhi ya mazao mbichi ya shambani katika duka la Jeff Mundia, Nairobi Farmers Market, Kiambu Road, kiungani mwa jiji la Nairobi tayari kusindikwa kuwa juisi…PICHA/ SAMMY WAWERU.

“Huunda juisi itokanayo na matunda, miwa na viungo vya mapishi,” aelezea.“Hivyo basi, hutusaidia kudhibiti kero ya mazao kuharibika,” Jeff aongeza. Wana mashine kadha za shughuli hiyo.

Duka hilo ambalo ni sawa na kiwanda cha kutengeneza sharubati, lina wafanyakazi kadha.Akisifia mpango huo, Jeff anasema ukiigwa na wakulima na wafanyabiashara wa mazao mbichi ya shambani utawasaidia kukwepa hasara ya kuharibika na kuoza.

Pauline Kainyu ni mfanyabiashara eneo la Lang’ata, jijini Nairobi na hutengeneza juisi na maziwa ya mtindi (yoghurt) kutokana na mazao mbichi ya shambani.Mbali na mashine ya kusaga matunda, pia ana ya kukama juisi kutoka kwenye miwa.

“Licha ya kuokoa mazao yasiharibike, yanapoongezwa thamani bei huongezeka,” Pauline asema.Aliingilia biashara ya kuunda juisi na kuuza bidhaa za kula mwaka uliopita, 2020 Kenya ilipokumbwa na Homa ya Corona.

“Nilikuwa katika sekta ya mapishi na iliathirika pakubwa kufuatia amri ya watu kukongamana ili kudhibiti msambao wa Covid-19.“Nilianza kwa kuuza bidhaa za kula na mazao mbichi ya shambani na ambayo yalikuwa yanaharibika yakikosa wanunuzi, ndiposa nikaibuka na mpango wa kuyaongeza thamani,” afafanua.

Mpango wa kuongeza mazao mbichi thamani hata hivyo haukosi changamoto zake, endapo mkulima au mfanyabiashara hana vihifadhio.Baada ya kusindika mazao, ni muhimu vinywaji vihifadhiwe vyema kwa kutumia jokofu (friji), chombo ambacho ni ghali hasa kwa watangulizi biashara.

  • Tags

You can share this post!

EPRA yashikilia kuwa ushuru na bei ya mafuta ng’ambo...

Ripoti yaibua wasiwasi kuhusu utunzaji wa nguruwe