• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
Mlalamishi aokolewa kukwepa genge linalohusishwa na washtakiwa wa wizi wa mabavu

Mlalamishi aokolewa kukwepa genge linalohusishwa na washtakiwa wa wizi wa mabavu

NA SAMMY KIMATU

MLALAMISHI katika kesi ya wizi wa mabavu aliokolewa na kituo cha Mukuru Promotion Centre (MPC) baada ya kuvamiwa na genge linalohusishwa na washtakiwa wakuu katika kesi hiyo.

Maafisa wamesema wanachunguza kubaini kama shambulio hilo ni la ulipizaji kisasi.

Mlalamishi David Safari alikosa kufika kortini Makadara wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo baada ya wanaume watano kumshambulia nyumbani kwake eneo la Budalangi katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba, South B, kaunti ndogo ya Starehe.

Mkurugenzi Mkuu wa MPC Mtawa Mary Killeen aliambia Taifa Leo kwamba Bw Safari alinusurika kifo kwa tundu la sindano kutoka mikononi mwa wahalifu hao.

“Alikuwa akitiririkwa na damu nyingi kichwani baada ya kuvamiwa na washukiwa. Isitoshe, waliharibu laputopu iliyokuwa nyumbani kwake. Tumemuokoa na kumtoa Kayaba na sasa yuko pahala salama katika kituo kimoja cha kurekebisha tabia,” Mtawa Killeen akasema.

Kwa mujibu wa mkuu wa polisi eneo la Makadara Bi Judith Nyongesa washukiwa watano walikamatwa katika mtaa wa Kayaba kuhusiana na kisa hicho.

“Polisi walikamata washukiwa watano akiwemo mwanamke anayeaminika kutafuta soko la bidhaa za kielekroniki zinazoletwa na washukiwa nyumbani kwake eneo la Budalangi,” Bi Nyongesa akasema.

Miongoni mwa vitu vilivyopatikana ni pamoja na kamera, tarakilishi, simu, visu na ,apanga miongoni mwa vingine kutoka kwa washukiwa hao.

Linalokera na kushangaza wakazi mtaani Kayaba ni kuwaona washukiwa hao wakiwa huru huku wakifuatilia kwa makini kubaini ni jinsi gani washukiwa hao walivyotoka ndani ya seli za polisi.

Mwishoni mwa juma lililopita, wakazi waliojawa na hasira walimshambulia na kumuua mshukiwa wa ujambazi aliyedaiwa kumpora mkazi wa mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba simu yake, alipokuwa akielekea nyumbani usiku.

Vilevile, kamanda Nyongesa alisema visa vyote viwili vinachunguzwa na polisi.

  • Tags

You can share this post!

Katuni, Oktoba 4, 2023

Wito kwa walioambukizwa HIV wajitokeze waziwazi kuepusha...

T L