• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Mshukiwa wa uhalifu chini ya mtandao wa ‘Jeshi ya Gaica’ hatimaye atiwa mbaroni

Mshukiwa wa uhalifu chini ya mtandao wa ‘Jeshi ya Gaica’ hatimaye atiwa mbaroni

Na MWANGI MUIRURI

MSHUKIWA wa uhalifu mjini Maragua katika Kaunti ya Murang’a na ambaye aliponea kupigwa kwa risasi wiki jana alipofumaniwa akilisha vijana watatu kiapo cha ujambazi alikamatwa Jumapili akiwa amejificha mvunguni mwa kitanda chake.

Idara ya polisi ilikuwa imeahidi zawadi ya Sh50,000 kwa yeyote ambaye angesaidia kukamatwa kwake.

Maafisa wa polisi ambao wamekuwa wakimfuata John Ngugi Maina ambaye kijiji chake ni Maica Ma Thi na ambaye inadaiwa ni kinara wa genge linalofahamika kama ‘Jeshi ya Gaica’ walinyemelea kwake na kuvunja mlango alipokataa kujisalamisha na wakamtwaa kutoka mvunguni. Ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na pombe haramu aina ya chang’aa kiasi cha lita 20.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kusini Bw Anthony Keter, usaidizi mkubwa wa kumnasa baada ya kuhepa mitego ya polisi kwa miaka miwili sasa ulitokana na ulevi.

“Mshukiwa huyo ambaye tulikuwa tunamuwinda ili ajibu mashtaka ya wizi wa mabavu, mashambulizi ya mauaji, upishi na uuzaji wa Chang’aa, matusi kwa wake wa wenyewe na kwa wengine akijaribu ubakaji na pia kuwa mfuasi na msajili wa magenge yasiyokubalika kisheria alitembelea bibi yake usiku wa Jumamosi akiwa mlevi.

“Aliingia kwake akiwa mlevi. Alianza kuiba nyimbo ya kivita katika ulevi huo. Hata yeye na ukora wake alikuwa amesherehekea sikukuu ya Pasaka vilivyo. Ndio majirani walimtambua na tukapokea simu tano za kutupasha habari. Tukamwendea,” akasema.

Bw Keter alisema kuwa aliyepiga simu ya kwanza ndiye alipokezwa zawadi ya Sh50,000 huku wengine wanne wakipokezwa Sh2,000 kila mmoja.

Bw Maina pia amekuwa akiongoza genge lake kuvamia mji wa Maragua na kuhangaisha wafanyabiashara na kwa wakati mmoja akamtisha Naibu Chifu wa mji huo Bw James Gachanja.

Alinukuliwa akimwambia chifu huyo kwamba “usiwahi kuonekana ukitekeleza majukumu yako katika ngome hii yangu kwa kuwa sisi ndio serikali ya hapa na ukikaidi tutakuadhibu vibaya sana.”

Bw Keter alisema kuwa mshukiwa amekuwa akiponyoka mitego tele ya maafisa wa polisi, katika hali nyinginezo, akiponyoka katika njia zinazoashiria kuwa alikuwa akipashwa habari za msako kumhusu na maafisa watukutu “lakini hatimaye busara imesimama na haki itatendeka.”

Bw Keter aliwataka wote ambao washawahi kudhulumiwa na mshukiwa huyo wajitokeze katika kituo cha polisi cha Maragua kuandikisha taarifa zao ili mashtaka dhidi yake yawe thabiti.

Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Bw Mohammed Barre alisema kuwa kukamatwa kwa Maina ni hatua kubwa sana katika usalama wa eneo hilo kwa kuwa alikuwa na mazoea ya kujaribu kusajili vijana wa umri mdogo katika maisha ya uhalifu.

“Kwa mwaka mmoja sasa kero katika eneo hili imekuwa ni huyu John Maina. Kuna wengine wawili ambao ni washirika wake na ambao ni Abraham Nduba na pia Peter Njeri ambao bado wako huru. Hata wao wanahitajika kwa kuwa kusafisha eneo hilo uchafu huo wa ujambazi, ni lazima wenyeji wathibitishiwe kuwa serikali ina mkono mrefu na maarifa ya kuwaandama wote wanaohujumu usalama,” akasema.

Bw Barre alisema kuwa serikali imejituma kuhakisha kuwa usalama umedumishwa katika kijiji hicho cha Maica Ma Thi ambacho kinafahamika kwa riziki ya kupika na kuuza chang’aa tangu taifa lijinyakulie uhuru na ni kazi ambayo imekuwa ikipokezanwa kwa vizazi vya familia hiyo.

Mshirikishi wa Masuala ya Kiusalama ukanda wa Kati Bw Wilfred Nyagwanga aliwapongeza maafisa waliomnasa Maina akiwataka pia kutia bidii kuwaandama waliobakia.

“Machi nilikuwa nimewapa maafisa wa kaunti hiyo ndogo wiki mbili wawe wamefagia uchafu huo wote wa ujambazi kutoka eneo hilo la Lokesheni ya Ichagaki. Siku zimesonga sana na tunataka tumalizane na kazi hiyo tushughulikie mengine ya maana kama ya kuwasaidia wenyeji kuafikia malengo ya kuboresha maisha yao,” akasema.

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa smoothie ya ndizi na parachichi

Onyo kwa wahudumu wa afya wanaoingiza ufisadi katika utoaji...