• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Onyo kwa wahudumu wa afya wanaoingiza ufisadi katika utoaji wa chanjo

Onyo kwa wahudumu wa afya wanaoingiza ufisadi katika utoaji wa chanjo

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI imetoa onyo kali kwa wahudumu wa afya wanaosakata ufisadi katika utoaji wa chanjo ya virusi vya corona.

Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya, Dkt Mercy Mwangangi alisema wizara imepokea malalamishi kuhusu wahudumu wa afya wanaoitisha hongo ili kutoa chanjo.

Dkt Mwangangi alionya watakaopatikana na hatia kuhusika wataadhibiwa kisheria.

Waziri alisema leseni zao zitafuliwa mbali, na kushtakiwa.

“Tumepokea ripoti baadhi ya vituo na wahudumu wanapokea hongo kuwapa watu chanjo, ili wasipige foleni. Watakaopatikana na hatia kuhusika, tutawachukulia hatua kisheria,” Dkt Mwangangi akatangaza.

“Kwa wahudumu wanaoshiriki kitendo hicho haramu, tutafutilia mbali leseni zenu,” akaonya.

Kaunti ya Nakuru, baadhi ya wakazi waliojitokeza kupokea chanjo katika vituo mbalimbali wamelalamikia ufisadi kusakatwa na hata kuitishwa hongo.

Chanjo ya AstraZeneca na inayoendelea kutolewa nchini, haina malipo yoyote.

“Inapatikana bila malipo katika vituo vyote vya afya; umma na kibinafsi, vilivyoidhinishwa kuisambaza,” akasisitiza Dkt Mwangangi.

Onyo hilo linajiri wakati ambapo taifa limeanza kushuhudia upungufu wa chanjo hiyo.

Serikali hata hivyo imehakikishia taifa kuwa itapokea dozi nyingine kufikia Mei 2021.

Usalama wa AstraZeneca umeanza kutiliwa shaka baada ya baadhi ya watu walioipokea katika bara Ulaya kufariki, vifo vyao vikihusishwa na chanjo hiyo.

You can share this post!

Mshukiwa wa uhalifu chini ya mtandao wa ‘Jeshi ya...

Aliyenaswa kwa video akimtesa mshukiwa wa wizi Ajab Mills...