• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mshukiwa wa unajisi aponea kuteketezwa Kambi Moto

Mshukiwa wa unajisi aponea kuteketezwa Kambi Moto

Na SAMMY KIMATU

KULIKUWA na kizaazaa kwenye eneo la Kambi Moto mtaani Kayaba, tarafa ya South B, kaunti ndogo ya Starehe polisi walipomwokoa mshukiwa wa unajisi.

Ilibidi maafisa wa polisi kutoka kituo cha South B kufika haraka kwenye eneo la kisa kumwokoa mshukiwa baada ya wakazi kuamua kumteketeza.

Aidha, inadaiwa Bw Nicholas Mavindu almaarufu ‘Baba Jomba’, 60, alimnajisi msichana wa umri wa miaka minane aliye katika Gredi ya Tatu na anayesomea katika shule moja iliyoko mtaani humo.

Inasadifu kwamba ‘Baba Jomba’ ndiye mwenyekiti wa Kambi Moto anayehudumu katika ofisi ya chifu wa Landi Mawe.

Maafisa wa watoto wa kujitolea mitaani wakishirikiana na wenzao wa afya ya jamii walisema mshukiwa alimwambukiza mtoto huyo maradhi hatari.

“Awali, mshukiwa alikuwa akimfanyia hivyo mtoto huyo mara kadhaa akimpa Sh200 na kumshawishi asieleze yeyote. Lakini siku zake arobaini zilitimia leo mshukiwa asijue alikuwa amewekewa mtego na maafisa wa watoto, polisi na vijana wa mtaa huo. Alichomolewa akiwa chini ya kitanda nyumbani kwa mpango wake wa kando,” Bi Victoria Wangui, 30, akasema.

Vijana kwa akina mama waliokuwa na hasira za mkizi walijaribu kuchukua sheria mikononi wakitaka kumteketeza mshukiwa.

Lakini maafisa wa polisi walikuwa chonjo na kumkamata na kumwondoa haraka kutoka kwa maficho yake na kumpeleka kituoni katika mtaa wa Hazina.

Shughuli zilisimama kwa muda mtaani huku mkuu wa tarafa, Bw Michael Aswani Were akilazimika kutoka ofisini kuwatuliza wananchi.

Hali ya taharuki ilitanda nje ya ofisi wakazi wakitaka wapewe mshukiwa wamteketeza.

Vile vile, walidai maafisa watatu wa masuala ya watoto hawakuwajibika hapo awali baada ya kupashwa ripoti kuhusu kudhulumiwa kwa mtoto na ‘chairman’.

Ilimbidi Bw Were akisaidiwa na maafisa wa polisi kuwaamrisha kusimama na kuondoka kutoka kwenye viti walivyokalia nje ya ofisi yake.

Ripoti ya daktari kutoka hospitali ya Mater ilionyesha mtoto alitendewa unyama na kuambukizwa maradhi na vile vile kuharibiwa vibaya katika sehemu zake nyeti.

Hatimaye, mtoto alichukuliwa na ambulensi na kupelekwa kwa matibabu maalumu.

Kadhalika, Bw Were alisema polisi wanawaska washukiwa wengine wawili waliotoroka na ambao wanahusika pia kushiriki kumdhulumu mtoto mwathirika.

“Serikali itamchukua mtoto imlee na kumtunza akiwa katika makao ya watoto kwa sababu mamake ana ulemavu wa akili na sheria haimkubalii kukaa na mtoto huyo aliye kitinda mimba katika familia ya watoto watano. Isitoshe, mama huyo hafanyi kazi ila hutegemea kusaidiwa na majirani na jamii miongoni mwa wengine,” Bw Were akanena.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Ushuru zaidi ni mzigo usiofaa

PATA USHAURI WA DKT FLO: Ukuvu mdomoni ni ishara ya HIV?