• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 7:55 PM
Joshua Arap Sang apendekeza Eric Omondi apelekwe kituo cha kurekebisha tabia

Joshua Arap Sang apendekeza Eric Omondi apelekwe kituo cha kurekebisha tabia

NA SAMMY WAWERU

MTANGAZAJI tajika wa redio Joshua Arap Sang amependekeza mcheshi Eric Omondi apelekwe katika kituo cha kurekebisha tabia na maadili.

Kulingana na mtangazaji huyo wa awali wa kituo cha Emoo FM, tabia za msanii huyo za hivi punde zinaashiria Mkenya anayepaswa kupitia hatua za kurekebisha tabia.

Bw Arap Sang alitoa kauli hiyo kufuatia kukamatwa kwa Eric mapema wiki hii, katika barabara ya Kenyatta Avenue, jijini Nairobi ambapo aliongoza kundi la vijana kuandamana kushinikiza serikali kupunguza gharama ya juu ya maisha.

“Huyu anahitaji Rehabilitation Centre sio kortini,” mwanahabari huyo akaandika, kupitia mchango wa chapisho la Facebook lililoangazia taarifa ya mchekeshaji Eric Omondi akiwa mahakamani.

Msanii huyo alifumaniwa na maafisa wa polisi kukabiliana na ghasia, mnamo Jumatatu ambapo alikuwa amefunga barabara kwa vizuizi.

Isitoshe, alikuwa anapiga mayowe askari waliokuwa ngangari jijini kuimarisha usalama wakimnyanyua na kumpeleka seli.

Eric Omondi (kushoto) akiwa kortini kwa kuzua vurugu. Picha / Richard Munguti

Eric Omondi alishtakiwa kusababisha vurugu kwa kuweka kizuizi barabarani, na kuwazuia watumizi wengine wa barabara.

Hata hivyo, Omondi alikana mbele ya hakimu mwandamizi Bi Zainabu Abdul kwamba alisababisha vurugu kwa kupiga kelele kuhusu bei ya unga.

“Mheshimiwa nimeshtakiwa kwa nini ilhali Kipengele 37 cha Katiba kinaruhusu maandamano na kupiga kelele ikiwa haki imekandamizwa?” Omondi alishangaa kortini.

Pia alieleza masikitiko kwamba ameshtakiwa ilhali muungano wa Azimio na serikali ya Kenya Kwanza ulikubaliana kusitisha maandamano na hata wanasiasa walioshtakiwa Kiambu waliachiliwa.

Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh5, 000 hadi Aprili 13, 2023 kesi itakapotajwa.

Si mara ya kwanza Eric Omondi kukamatwa kwa kuzua zogo jijini Nairobi, na kufunguliwa mashtaka.

  • Tags

You can share this post!

Bunge lachunguza usafirishaji wa mibuyu ng’ambo

City Mortuary kuzindua makafani maalum ya matajiri

T L