• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Mtu mmoja afa kwenye ajali mbaya ya barabarani Nakuru

Mtu mmoja afa kwenye ajali mbaya ya barabarani Nakuru

NA JOHN NJOROGE

MTU mmoja alifariki kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea eneo la Twin Bridge, kwenye barabara kuu ya Eldoret-Nakuru, Kaunti ya Nakuru, Jumamosi, Oktoba 21, 2023 usiku.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kuresoi, Bw Juddah Gathenge, alisema ajali hiyo iliyoyokea saa tatu usiku, ilihusisha trela na lori ambazo zilikuwa zikielekea pande tofauti.

“Trela lilikuwa likielekea upande wa Nakuru kutoka Eldoret, wakati lilipogongana na lori lililokuwa likielekea Eldoret. Wakati wa ajali hiyo, mtu mmoja aliaga dunia akipelekwa hospitalini huku wengine watatu wakijeruhiwa vibaya,” alisema Bw Gathenge, akiongeza kuwa waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Molo kupokea  matibabu.

Akizungumza na Taifa Jumapili kwa njia ya simu, mkuu huyo wa polisi alisema marehemu alikuwa mmoja wa madereva huku walionusurika wakiwa abiria wawili na dereva wa gari lingine.

Alisema kuwa polisi wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo.  Bw Gathenge alitoa wito kwa madereva wa magari kuwa waangalifu hasa wanapoendesha magari nyakati za usiku.

“Tunakaribia msimu wa sikukuu hivyo nawaomba watumiaji wa barabara kuwa waangalifu hasa wanapoendesha gari nyakati za usiku ili kuepuka matukio ya aina hii siku zijazo. Nawaomba  kuzingatia sheria za barabarani,” alisema.

Mwili wa mwathiriwa ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Molo huku magari yaliyohusika ajalini yakikokotwa hadi kituo cha polisi cha Mau Summit yakisubiri kufanyiwa ukaguzi.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Bahati ‘Mtoto wa Mama’ kupambana na Sakaja ugavana...

Mashirika ya serikali yenye ‘mahema’ katika...

T L