• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
Bahati ‘Mtoto wa Mama’ kupambana na Sakaja ugavana Nairobi mwaka 2027

Bahati ‘Mtoto wa Mama’ kupambana na Sakaja ugavana Nairobi mwaka 2027

NA WINNIE ONYANDO

MWANAMUZIKI Kevin Kioko almaarufu Bahati ametangaza kuwa atawania kiti cha ugavana katika Kaunti ya Nairobi mwaka 2027.

Mwanamuziki huyo endapo atatimiza na kuweka hai ahadi hii, basi atapambana na gavana wa sasa wa Nairobi Bw Johnson Sakaja.

Bahati alitoa tangazo hilo akiwa katika Chuo Kikuu cha Zetech.

“Japo nilishindwa kupata kiti cha ubunge katika uchaguzi mkuu mwaka 2022, nina nia ya kuwania kiti cha ugavana ifikapo mwaka 2027,” Bahati alisema.

Mwanamuziki huyo pia aliahidi kuwa anajiunga na chuo kikuu hicho kwa elimu ya shahada ya kwanza.

Mwaka 2022, Bahati alitangaza nia yake ya kuwania kiti cha ubunge Mathare kupitia chama cha Jubilee.

Hata hivyo, mambo yalienda mrama na akalazimika kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Haijulikani ikiwa mwanamuziki huyo atanguruma kuliko Sakaja na wagombea wengine ambao huenda watajitokeza. Hii ni kwa sababu, umaarufu wa Bahati unatokana na muziki bali si siasa.

Haya yanakuja siku chache baada ya mwanamuziki huyo kutangaza kuwa anajitayarisha kufanya harusi na mpenziwe Diana Marua.

“Ni rasmi kuwa nimelipa mahari kwa Mzee Omach ambaye ametubariki ili tuendelee na maandalizi ya harusi,” alichapisha Bahati.

Bahati alisema kuwa aliamua kufunga rasmi pingu za maisha na Diana kutokana na kiu ya kutaka kuhalalisha ndoa yao.

Naye Diana alidokeza hakuwa anatarajia kulipiwa mahari tena, kwani msanii huyo alikuwa amefanya hivyo wakati wa maadhimisho ya miaka saba tangu wawili hao kuishi pamoja.

“Hii ni zawadi bora kutoka kwa yule Maulana alinijalia akanipa. Naahidi kufanya kulingana na mafundisho ya Biblia kwa kumpenda na kumheshimu siku zangu zote za maisha,” Diana alirusha ujumbe ulioelekezwa kwa Bahati.

  • Tags

You can share this post!

Madiwani wa UDA Nairobi wapanga njama kung’oa kiongozi wa...

Mtu mmoja afa kwenye ajali mbaya ya barabarani Nakuru

T L