• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mwanamke aangua kilio korti kuamua baba watoto alipie karo, matibabu pekee

Mwanamke aangua kilio korti kuamua baba watoto alipie karo, matibabu pekee

NA TITUS OMINDE

MWANAMKE  mmoja alisababisha kioja katika mahakama ya hakimu mjini Eldoret Ijumaa, Oktoba 6, 2023 bada ya mahakama kuamua kuwa mwanaume ambaye wamezaa naye watoto wawili atagharamia tu karo ya shule kwa watotoa hao wa umri wa kati ya miaka mitano na miezi tisa.

Mwanamke huyo alikuwa amefika mahakamani mapema mwaka huu akitaka mahakama ya watoto kumshurutisha mwanaume huyo ambaye ni mwalimu mkuu wa shule moja ya upili katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet kugharamia mahitaji yote ya watoto hao.

Hata hivyo, mahakama iliamua kuwa mwanaume husika atakuwa akigharamia tu karo ya shule na matibabu kwa watoto hao.

Uamuzi huo ulimghadhabisha mwanamke huyo wa umri wa miaka 25 na kuanza kupiga nduru mahakamani huku akidai kuwa uamuzi huo ulipendelea mwanaume.

“Hakuna haki, hakuna haki, nimedhulumiwa itakuaje mtu ambaye alipachika mimba nikiwa chuoni agharamie tu masomo ya watoto ili hali watoto wanahitaji chakula, mavazi na mahala pa kuishi. Huu ni ufisadi,” alisema mwanamke huyo huku akipiga mayowe kortini.

Kwa muujibu wa mama huyo ni kwamba, ingekuwa afueni iwapo mahakama ingemshinikisha mwanaume huyo awe akigharamia chakula na mavazi kwa watoto hao mbali na karo na kumpa angalau Sh5,000 kwa mwezi kukidhi mahitaji mengine ya watoto husika.

Alidai kuwa uamuzi huo haukuwa na uwazi.

Juhudi za walinzi wa mahakama kumtuliza ziligonga mwamba kwani aliendelea kupiga mayowe huku akitishia kutoa nguo zote.

“Ni heri nife nisiteseke na watoto wa mtu ambaye ameniachia mzigo wa ulezi,” alisema mwanamke huyo.

Alizuia mwanaume husika kuondoka kortini huku akitishia kuwa atampa watoto wote aende nao badala ya kugharamia masomo tu ili hali yeye ameachiwa mzigo mkubwa.

Hatimaye, mwanamume husika alimbeba mwanamke huyo kwa gari lake na kuondoka pamoja na watoto wao mahakamani.

Uamuzi huo ulitolewa na hakimu wa masuala ya watoto, hakimu mwandamizi, Christine Menya kupitia kwa mtandao.

  • Tags

You can share this post!

Waislamu na wanaharakati wataka majaji waliotoa uamuzi wa...

Kutana na Mzee Mohamed Mbwana Shee almaarufu ‘Kamusi...

T L